Taarifa nilizozipata kutoka kwa msiri wangu wa ndani ya Ikulu jijini Dar es Salaam anasema, serikali ya Rais Jakaya Kikwete tayari imefilisika. Haina fedha ya kuendeshea shughuli zake.

Aliyekuwa waziri wa fedha, William Mgimwa alinukuliwa akiwaambia Shirika la Fedha la Kimatifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB), kwenye mikutano ya mwaka ya WB na IMF iliyofanyika mjini Washington DC kuanzia tarehe 7 hadi 15 Oktoba 2013.

Waziri Mgimwa alisema, serikali imezidisha ukomo wa kukopa ndani wa Sh. 484 bilioni ambayo ndiyo iliyoruhusiwa kwa mujibu wa makubaliano na mashirika hayo na kulazimika kukopa nje ya makubaliano kiasi cha Sh. 1, 244.7 bilioni kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani.

Kwa mujibu wa msiri wangu, hali hii imeifanya serikali kuwa na wakati mgumu mbele ya mashirika ya kimataifa na kwa wafanyabiashara wa ndani. Deni la taifa sasa limefikia kiasi cha Sh.22 trioni (mwaka 2013) ambayo sawa na asilimia 42.5 ya pato la taifa.

Katika mikutano hiyo, msiri wangu amenieleza Waziri Mgimwa aliongozana na ujumbe ufuatao:

Omari Yusuf Mzee, Waziri wa Fedha (SMZ); Bi Liberata Mulamula, Balozi wa Tanzania Washington DC, Dk. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha; Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania; pamoja na maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango (SMT na SMZ); Ubalozi wa Tanzania Washington DC; Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Wengine, ni Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya SMZ; Dk. Philip Mpango, Harry Kitilya, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Amina Shaaban, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar.