Mjadala mkali umeibuka katika siku ya 11 ya Bunge la Katiba mjini hapa leo kati ya wajumbe wanaotaka kanuni ziruhusu kura ya siri na wale wanaotaka kura ipigwe kwa uwazi.
Dodoma. Mjadala mkali umeibuka katika siku ya 11 ya Bunge la Katiba mjini hapa leo kati ya wajumbe wanaotaka kanuni ziruhusu kura ya siri na wale wanaotaka kura ipigwe kwa uwazi.
Rasimu ya kanuni zitakazoongoza uendeshaji wa Bunge hilo iliyowasilishwa jana imeshauri wajumbe wapewe haki ya kupiga kura kwa siri, kama ilivyo katika mchakato wowote wa kidemokrasia.
Mapema leo, mwanasiasa machachari Christopher Mtikila aliunga mkono ushauri huo, akisema “Kura siku zote ni ya siri.” “Haina mjadala, kwa sababu ndio msingi wa demokrasia.”
“Lazima kura ya siri, manake sheria haitaki kushurutishana,” alisema mbunge wa Viti Maalum wa CCM, Esther Bulaya.
Wajumbe wengine, akiwemo mwakilishi wa taasisi za kidini, Sheikh Mussa Kundecha, wamesisitiza kuwa kura ya siri itawapa wajumbe nafasi ya kufanya maamuzi kwa uhuru.
“Kura ya siri ni muhimu sana ili kuwaacha watu wakiwa wamoja, na ndiyo itakayotutoa hapa tukiwa wamoja, tena kwa heshima,” alisema Sheikh Kundecha.
Hata hivyo, hoja hiyo ya kura ya siri ilipingwa vikali na baadhi ya wajumbe, akiwemo Zainab Gama, anayesema:
“Na unayetaka siri manake kuna mtu amekuleta hapa, au na rushwa ushakula sasa unaona aibu kutangaza.”
Kutokana na uzito wa mjadala huo wa kura, mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho, alilazimika kusogeza mbele muda wa kumaliza kikao hicho hadi saa tatu usiku.
Pamoja na hatua hiyo, Bunge hilo lilishindwa kupata muafaka kuhusu kura itapigwa vipi, wala kanuni zipi zitatumika kuliendesha.
Hali hii ililazimisha Bunge hilo maalum liahirishwe hadi Ijumaa, Februari 28, saa 11 jioni ili kuipa kamati inayoandaa kanuni nafasi ya kuzifanyia majumuisho mnamo asubuhi.