STRAIKA Mzambia, Felix Sunzu ameisikitikia klabu yake ya zamani ya Simba kwa matokeo mabaya inayopata na kusema inaponzwa na tabia ya kubadili timu kila wakati.
Sunzu ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Green Buffalose inayomilikiwa na Jeshi la Zambia, alikuwa kwenye kikosi cha Simba msimu wa 2011/12 na kuifikisha timu hiyo hatua ya tatu ya mtoano ya kufuzu makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sunzu alisema: “Nasikitika sana kwa matokeo ambayo Simba wanayapata, ni mbaya sana, maskini timu yangu.”
“Kwa nini inakuwa hivyo? Hawana fedha au ni nini? Lakini huenda inachangiwa na kitendo cha kubadili timu kila wakati,” alisema Sunzu.
Simba wikiendi iliyopita ilifungwa mabao 3-2 na JKT Ruvu katika Ligi Kuu Bara huku ikipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mgambo JKT.
Timu hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya City.