MAHASIMU wawili Mkurugenzi wa Aset inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta Asha Baraka na Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Chocky leo nusura wazichape kavukavu baada ya kutokea hali ya kutoelewana baina yao.
Tukio hilo lilitokea majira ya mchana, kwenye ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, jijini Dar es Salaam wakati mabosi hao walipokutana ghafla, kila mmoja akiwa kafika na hamsini zake.
Chanzo cha Saluti5 kilieleza kuwa, Chocky aliingia Mango na kumkuta Asha akiwa anazungumza na mdogo wake, Omari Baraka kwenye meza ya peke yao, ambapo aliwapita kwa amani bila kuwasemesha chochote.
Saluti5 inaambiwa kwa mshangao wa wengi dakika chache baadae wawili hao wakajikuta wako katika vita vikali vya maneno huku ikiwa haieleweki haswa nani aliyemchokoza mwenzake.
Vita vya maneno vilikuwa vikali kiasi cha kutaka kushikana lakini ugomvi ukaamuliwa na mwimbaji wa FM Academia Patcho Mwamba.
Saluti5 ilipomtafuta Patcho Mwamba kwa njia ya simu, alithibitisha kutokea kwa sintofahamu hiyo iliyotishia kuvunjika kwa amani.
Katika miezi ya hivi karibuni, wawili hao wamekuwa katika uadui mkubwa ambapo tarehe 11 mwezi Juni mwaka jana, Ally Chocky aliwahi kuimbia Saluti5 kuwa akifa basi Asha Baraka asiende kwenye msiba wake.
Asha Baraka naye katika siku hiyo hiyo kupitia Saluti5 akasema hayo ni mambo ya kike na kwamba Wamanyema wanatosha kumzika.
Pichani juu ni picha mbili tofauti zikiwaonyesha Chocky na Asha Baraka wakiwa kwenye mazishi ya dansa Mwantumu aliyezitumikia Twanga Pepeta na Extra Bongo.