Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,Ramadhani Mungi akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali,mapema leo asubuhi kwenye Ofisi zake,kuhusiana na mambo mbalimbali yaliyohusu kuelekea Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kalenga,mkoani Iringa.
======== ====== ===========
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Ndugu waandishi wa habari , kwa niaba ya askari Polisi wa Mkoa wa Iringa, nitumie fursa hii kuwakaribisha hapa ofisini kwetu.
Ndugu zangu tumeitana hapa asubuhi hii ili niweze kuwapa taarifa ya usalama katika Mkoa wetu wa Iringa hususani katika Jimbo la Kalenga katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kalenga na usalama wa siku ya uchaguzi wenyewe.Ili iwe rahisi kueleweka taarifa hii nitaitoa kwa kifupi sana kwa kuigawa katika maeneo matatu.
Eneo la kwanza ni juu ya wapi tunataka tupafikie ( Where we want to go ), eneo la pili ni lile la wapi tulipo ( Where are we? ) na eneo la tatu ni jinsi gani tutafika huko ( How do we get there ). Tuanze na wapi tunataka tupafikie. Sisi Polisi Mkoa wa Iringa tunataka wananchi wa Kalenga wapinge kura kwa amani na utulivu mkubwa siku ya jumapili tarehe 16/3/2014. Hii ndio dila yetu na tutahakikisha tunafika hapo.
Kuhusu wapi tulipo sasa, naomba niwaelezeni kwa ufupi sana matukio ya kijinai kuanzia tarehe 19/02/14 mpaka leo. Ndugu zangu, kuanzia tarehe hiyo mpaka tarehe 2/03/2014 takribani wiki mbili hakukuwa na tukio lolote la uvunjifu wa amani lililokuwa limepokelewa katika vituo vyetu vya Polisi.
Hali ilianza kubadilika tarehe 3/3/2014 ambapo baadhi ya waandishi walifika ofisi kwangu na kunieleza kuwa kumetoka kwenye mkutano wa CHADEMA ambapo wameelezwa na chama hicho kuwa usiku wa siku hiyo walimkamata mtu mmoja kwa kosa la kujaribu kuchoma moto nyumba waliokuwa wakiishi wafuasi wao katika kijiji cha WASA.
Waandishi hao walinitaka nithibitishe kutendeka kwa kosa hilo na walieleza kuwa wameelezwa kuwa bado halijaripotiwa kituoni. Mimi nilikataa kusema lolote kuhusu hilo kwani lilikuwa bado halijaripotiwa Polisi.
Tarehe 4/03/2014 nilifuatwa tena na baadhi ya waandishi na kunieleza kuwa siku hiyo waliitwa na CCM na kuelezwa kuwa siku ya tarehe 27/2/2014 walitegewa misumari katika kijiji cha WASA ili mabasi yaliyokuwa yamebeba wafuasi wao yaweze kutobolewa magurudumu yake, pia nao walisema tukio hilo halijaripotiwa Polisi. Mimi nilikataa kulizungumzia swala hilo.
Ndugu wanahabari, vitendo vilivyofanywa na vyama hivyo vililenga kuanzisha propaganda za kisiasa kwa kutumia uhalifu kwa kupitia vyombo vya habari. Sisi Polisi tulibaini hali hiyo na ndiyo sababu tuliamua kuwa kimya na nyinyi wenzetu kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu pia mlikaa kimya. Kuanzia hapo vyama vilianzisha mashindano ya kuripoti kesi zao Polisi. Leo hii vyama hivyo vimeripoti kesi ishirini na moja ambazo zilisababisha kukamatwa kwa wafuasi (19) wa vyama hivyo viwili.
Ndugu waandishi, kati ya kesi hizo ishirini na moja, kesi kumi na tisa (19) zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja kwa binadamu ama mali, kesi hizo ni zile ndogondogo sana, kama vile kuchana mabango, kuteremsha bendera, kuchana vipeperushi, kutukanana n.k. kesi tatu zilikuwa zile zenye madhara kwa binadamu na mali ambazo ni kupigana hadharani, kujeruhi na kuharibu mali. Kati ya kesi ishirini na moja (21), kesi kumi upelelezi wake umekamilika na majalada yake yamefikishwa kwa mwanasheria wa serikali.
Ndugu waandishi, katika kesi hizo Polisi tumeibaini mengi mfano CHADEMA kilikuwa kikitoa malamiko kuwa tumeacha kumkamata ndugu hassan mtenga mtuhumiwa wa kesi moja iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake. Shutuma hizo hazina msingi kwani kesi iliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo haikuwa ya jinai bali ya madai na tuliwajulisha hivyo. Nia ya kufanya hivyo ilikuwa kuifanya jamii iamini kuwa Polisi ni dhaifu na wenye kuonyesha upendeleo katika kushughulikia kesi za uchaguzi. Nashukuru Polisi tulikuwa watulivu, hatukujibu na jamii imetuelewa sana.
Ndugu waandishi, sijui mlijulishwa na nani kwamba Padri mmoja alifungwa kamba na alipingwa na kuburuzwa. Nanyi bila ya kuthibitisha kwetu mkaandika habari hiyo. Tuwaeleze kuwa mtu huyo ni miongoni mwa watuhumiwa tuliowakamata katika moja ya makosa yaliyotendeka, tulimhoji, aliandikwa maelezo yake na alipewa dhamana. Hata siku moja hajawahi kutoa taarifa Polisi juu ya matukio aliyotendewa. Nia ya kutangaza taarifa hiyo ni kuzua hofu kwa wananchi na kutaka kuchochea chuki kwa wafuasi wa dhehebu lake na wale wa dini yake.
Ndugu waandishi, pamoja na matukio hayo polisi tumekuwa tukipokea taarifa za vitisho vya kuwepo kwa watu mbalimbali kutoka kwa vyama vyote walioingizwa mkoani humu kwa nia ya kutenda vitendo vya uvunjifu wa amani. Aidha, tumewasikia viongozi wa vyama wakitamba kuingiza maelfu ya watu mkoani mwetu. Kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura.
Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa, kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndio wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni askari wa Jeshi la Polisi.
Kufuatia hali hiyo mambo yafuatayo yanasisistizwa sana.
1. Hatutaki kuona walinzi wa chama chochote katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la JESHI LA POLISI.
2. Hatutaki kuona watu wasiokuwa na shughuli maalumu wanapitapita katika maeneo ya kupigia kura.
3. Siku ya uchaguzi si siku ya kampeni. Hatutaki kuona helikopita za vyama vyote zenye kuashiria kufanya kampeni.
Nawaasa watu wote hasa wale waliotoka nje ya Iringa, sisi huku Iringa tunapenda sana amani kuliko kitu chochote kile hivyo ikiwa wameletwa kama MAJESHI YA KUKODIWA ili kuharibu amani ya Kalenga kama walivyozoea kufanya huko walikotoka, Sisi Polisi na wana Kalenga tupo imara, tumejipanga vizuri kukabiliana nao.
Aidha, napenda kuwatoa hofu wana kalenga, wasiwe na wasiwasi kabisa, sisi Polisi Iringa tupo imara na tumejipanga vizuri katika kuwalinda kikamilifu. Nawaomba wajitokeze kwa wingi sana siku ya kupiga kura na wapige kura zao kwa uhuru kabisa.
Ndugu waandishi, nawashukuru sana kwa jinsi mlivyofanya kazi zenu kwa ueledi mkubwa. Hata siku moja hatujawahi kusikia ama kusoma habari za uchochezi kwa kushabikia chama chochote kile.
AHSANTENI SANA.