BUNGE LETU LA KATIBA DODOMA NDIO TAIFA LETU LA SASA.
Bunge la katiba Dodoma limekuwa likikutana kwa takribani siku 18 sasa kupitia rasimu ya Katiba mpya, hesabu za haraka haraka zinaonyesha kwamba toka mchakato mzima wa Katiba uanze kitaifa tumeshatumia jumla ya Shillingi Billioni 92 kwa maana ya Billioni 70 za Tume ya Warioba, Billioni 8 za kukarabati Bunge jipya maalum la Katiba na Billioni 3.5 zilizokwisha tumika toka Bunge hilo lianze kukutana Dodoma. Hesabu zinazotisha zaidi ni zile zinazo onyesha kwamba kila siku ya iendayo kwa Mungu, Bunge hilo hutumia jumla ya Shillingi Millioni 190 kwa ajili ya posho tu za Wabunge 640 ambao hulipwa jumla ya Shillingi Laki tatu (300,000) kwa siku na hesabu hii ya ujumla wa siku sio pamoja na shughuli nzima ya gharama ya kuendesha bunge hilo kwa ujmla wake kila kila siku toka lianze siku 18 zilizopita.Demokrasia ni gharama sana kuwa nayo na hasa kuianza lakini ni muhimu sana gharama hizo zikawa na uwajibikaji ambao bado wananchi wengi hatujauona toka bunge hili kuanza Dodoma.
Toka kuanza kwa Bunge kumetokea malalamiko makubwa toka kwetu wananchi juu ya mambo mengi yaliyokwisha fanyika na yanayoendelea kufanyika ndani ya vikao vya bunge hilo kwamba hayafanani na sisi wananchi wa sasa wa Tanzania na wengi wetu tunaamini sana kwamba iwepo tungepata nafasi hiyo tungekwenda Dodoma na kufanya mambo tofauti sana na yale yanayofanyika huko bungeni sasa hivi. Ukweli wa mambo ni kwamba matatizo yalianza toka siku ya kwanza ya kuanza kwa kikao, tatizo la kwanza lilikuwa ni posho za wabunge, la pili likaja namna ya kupiga kura kama ziwe za wazi au za siri, na wiki hii likazuka tatizo la uvaaji ndani ya bunge, yote haya ni mbali kabisa na mawazo yetu wananchi wengi tuliokuwa tunalisubiri kwa hamu bunge hili la kurekebisha Katiba yetu ya Jamhuri ambayo tumeililia kwa muda mrefu sana kwamba ilihitaji marekebisho.
Baada ya kufuatiilia kwa makini sana kila kitu kilichokwisha fanyika na kinachoendelea sasa hivi Dodoma, ninatatizwa sana na ukweli kwamba Wananchi wengi wanaolalamikia tabia wa wabunge wa Bunge hilo kushindwa kuelewa alama za nyakati na hasa nyakati za mabadiliko za tabia zetu wananchi wa Tanzania za kupitia kipindi cha mabadiliko makubwa sana kama sio mapinduzi ya kitabia ambayo taifa hili tunapitia sasa hivi. Kinachoendelea Dodoma ni ukweli usiopingika kwamba ndio Tabia zetu mpya wananchi wa Taifa hili sasa na wabunge wetu kule wanatuwakilisha ipasavyo bila hata ya kukosea na kama kawaida ya binadam huwa ni rahisi sana kuona kibanzi kwenye jicho la mwenzio lakini sio kibanzi kile kile kilichoko machoni mwako ndio maana kumekuwa na makelele makubwa sana toka kwetu wananchi huku wote tukiwa hatuna kabisa jawabu la haraka au mkato la nini kifanyike na nini kisifanyike kama kweli tunataka Katiba bora na njema kwa Taifa letu la sasa na lijalo.
Katika Miaka ya karibuni Tanzania tumejikita kwenye siasa zinazo ongozwa na misingi ya kiuchumi zaidi, na kwa sababu hiyo sasa wananchi wengi tunaongozwa na mawazo ya kifaida zaidi kuliko yale yaliyokwisha pitwa na wakati ya kisiasa zaidi na maadili. Bado wananchi wengi tunashindwa kukubali kutokana na kutokujua kwamba zile enzi za kuongozwa na chama kimoja cha siasa zimekwisha siku nyingi sana na sasa tunaongozwa na siasa za vyama vingi, kimsingi dhana hiyo tuliipata kutokana na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kikiwa ni kiashirio kwamba siasa za kibepari ndio zilizoshinda katika vita kali ya baridi au "Cold War" na kwamba moja ya sheria namba moja ya siasa zilizoshinda vita ile ni Taifa kuongozwa na vyama vingi vya siasa na kufuatia kwa mengineyo hasa kubwa likiwa ubinafsi ambao siku zote huambatana na umaarufu wa binadam mmoja mmoja.Ndio maana tatizo kubwa la kwanza la Bunge hili Dodoma lilikuwa ukubwa na udogo wa posho za wabunge ni kwa sababu wabunge wetu wapya huko Dodoma ni wale wale yaani sisi wananchi wa Tanzania ambao sasa tunaongozwa zaidi na siasa za kiuchumi zinazojali faida kwanza kabla ya mengine yote.
Zile enzi za jamii iliyojali maadili zaidi ya akina Mwabulambo, Kaduma, ELy Anangisye, Sozigwa, Kawawa, Elinawinga, Lawi Sijaona, Amir Jamal, Dr. Kleruu na wengineo sasa zimeisha ni bora Taifa hili na hasa viongozi wa Taasisi mbali mbali za taifa na hasa Viongozi wetu wa dini mbali mbali nchini wakalielewa na kulikubali hilo kuliko kujairbu kushindana nalo kama ambavyo wamekuwa wakipiga kelele kubwa ambazo ndani yake hazina mashiko kabisa wala majawabu ya tatizo lililopo Dodoma ndani ya bunge la letu la Katiba. Kwa mfano Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba Mhashamu Kilaini, yeye aliwashambulia Wabunge wazoefu kwamba ndio tatizo ndani ya bunge hili jipya na huku Shehe Mkuu wa Dar akiwalaani Wabunge wote kwa kukosa uvumilivu, naye Mjumbe wa Tume ya Rasimu Professor Baregu, akilalamikia muda unaopotezwa bure huko Dodoma. Ukiwasoma kwa makini hakuna hata mmoja wao anayeonyesha kuelewa tatizo la bunge hilo Dodoma, wote wamerusha matamko ambayo ni hewa tupu ambayo haiwezi kusaidia kitu chochote kubadilisha mawazo ya wabunge wa bunge hilo la Katiba.
Ukweli ni kwamba kinachoendelea Dodoma ndio hasa mwangwi wa kinachoendelea kwenye vichwa vingi vya wananchi wa Tanzania sasa hivi, malumbano makubwa yanayoendelea pamoja na wengi wao kusimamia hoja zisizo za msingi sana kwenye kuelekea kurekebisha katiba yetu ni kutokana na misingi mipya inyotuongoza kimaisha sasa hivi Taifa hili. Huwezi kuamini siasa za kiuchumi bila ya kuamini katika umaarufu wa binafsi wa mwananchi, sasa unaupataje umaarufu katika bunge la siku 70 tu kurekebisha katiba ya jamhuri? Ni kwa kuanzisha mabishano yasiyokwisha bila hata kujali hoja za kimsingi za Katiba, na ukweli upo wazi kabisa katika suala zima la marekebisho ya katiba yetu kwamba hatujwahi kuwa na makubaliano ya hiari huko nyuma ya nini hasa tatizo la Katiba yetu ya zamani na sheria ya maisha ipo wazi sana kwamba kama hujui unakotoka huwezi kujua unakokwenda.
Binafsi, sijawahi kusikia hoja nzito na za kimsingi zikizungumzwa na wananchi wa Tanzania na hata Viongozi wetu za tatizo la kimsingi la Katiba yetu ya zamani lipo wapi. Matokeo yake tumeishia kusikia sana hoja ya Serikali Tatu na Mbili ikitawala karibu magumzo yote yawe rasmi na hata yasiyo rasmi kuhusiana na marekebisho ya Katiba. Ni vipi Serikali Tatu au mbili ni tatizo kwa Mwananchi wa kawaida anayehangaika kutatuta milo mtatu kwa siku na kukutana na vikwazo kila kona ya maisha yake na hata kufikia kuuziwa unga au mchele ulioharibika kwa makusudi na wafanya biashara wahuni ambao hakuna sheria nzito za kuwabana wanapofanya vituko kama hivyo. Tumesikia tatizo kubwa la baadhi ya wafanya biashara wa mafuta nchini wanavyochanganya mafuta na maji au mafuta ya taa kila wakati na hata wakati mmoja wakaufanyia msafara wa Rais wa jamhuri mikoani, je ni nini dawa mpya ya Kisheria ya watu wa namna hii? Lakini kwa mshangao mkubwa sana hoja iliyokuwa ikipigiwa kelele sana na wahusika kuelekea bunge hili ni Serikali Tatu tu ambayo na yenyewe ukichimba sana kwa chini yake kinacholiliwa ni madaraka tu ikiwa ni ile ile dhana ya ubinafsi ambayo inalitingisha sana bunge letu la KAtiba sasa hivi Dodoma.
WaTanzania tufike mahali tukubali kwamba tumebadilika sana na ndio maana siku moja pale UWanja wa Taifa Dar tulifikia mahali pa kujaza Uwanja ule kwa kiingilio tena kikubwa sana kwa ajili tu ya kwenda kuangalia pambano la ngumi baina ya kina dada wacheza cinema wa Bongo Muvi, Jacky Wolper na mwenzake Wema Sepetu. Sasa cha ajabu zaidi ni kwamba kati ya wananchi 65,000 waliokuwa wameijaza Uwanja siku hiyo ya ngumi hizo za wanadada hao Asilimia Sitini na Tano ni wapiga kura kwenye uchaguzi ujao wa Rais na Wabunge. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuishia kuchagua viongozi wanao fanana nao kimawazo na kulipelekea Taifa letu kwenda mrama zaidi na Uongozi wa Taifa. Lakini bado mwisho wa yote ni kwamba ni sisi wenyewe wananchi wa Tanzania ya sasa wapenda simu za kisasa za mikononi, Facebook, Twitter, Skype na Watsap na vyombo vya elektroniki na umaarufu wa haraka haraka kwa sababu unalipa sana tena kwa haraka haraka. Tanzania ya leo tuna Mwanamuziki kama Diamond Platznum, hana bendi maalum kama MSondo na Sikinde yeye huimba peke yake kwa kutumia muziki wake alioutengeneza mwenyewe Studio na kuuweka kwenye CD, lakini katika kipindi cha miaka minne iliyopita amelipwa hela nyingi sana kuliko hela walizokwisha wahi kulipwa wanamuziki wote wa Taifa hili ukiwachanganya kwa ujumla wao toka tupate uhuru. Ndio faida ya umaarufu wa haraka haraka ambao siku zote unakuzwa na kusambazwa kwa haraka sana kwa kutumia vifaa hivi vya elektroniki ambavyo sio siri wananchi wote sasa hivi tunavipenda sana hili Taifa.
Kwa kumalizia naomba kusema kwamba tusiwashambulie sana wabunge wetu wa Katiba Dodoma, isipokuwa tuwape nafasi ya kufanya wanachokiweza kwa kuongozwa na Sheria zilizopo za Jamhuri. Tutafute uelewa zaidi wa kutufungua vichwa vyetu wananchi ili kuelewa kwamba hata sisi ambao hatukuchaguliwa kwenda huko Dodoma, tungechaguliwa tungefanya hayo hayo wanayoyafanya wenzetu huko kwa sababu wao ni wale wale yaani sisi wananchi. Wabunge wetu Bunge la Katiba Dodoma hawakutoka Mbnguni moja kwa moja au ni Malaika flani hivi, hapana ni sisi wenyewe wananchi wa Tanzania kwa hiyo ni muhimu tukakubaliana na wakati kwamba umebadilika na sasa tutumie wakati tulionao kufanya tunayoweza na kwa vile kwenye taifa hili hili bado tunao wachache wanaoweza kutukumbusha kukaa kwenye mstari, basi tuwape nafasi ya kuwasikiliza watusahihshe ingawa tatizo linakuja pale wanapo onekana kama na wao hawana maadili mazito kama sisi wananchi.Hakukuwa na sababu yoyote ya Tume ya Warioba kukomalia sana Serikali Tatu, kwani ni kule ndiko waliko panda mbegu za malumbano toka wakitengeneza Rasimu hiyo, sasa wasishangae kuona malumbano walioyaanza wenyewe kule Tume yao, yamehamia Bungeni. Kinachoendelea Dodoma sasa hivi ndani ya bunge la katiba ni mwangwi tu wa sisi wananchi wote wa Tanzania tupo sawa sawa nao wabunge wetu. MUNGU IBARIKI TANZANIA
WILLIAM J. MALECELA + 255717618997 williammalecela.blogspot.com/willymalec@gmail.com |