MAALIM SEIF |
Walimtaka kiongozi huyo arudi kijijini kwake Mtambwe mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana na kuzidisha kile walichodai ni siasa za uongo, uzushi na uzandiki.
Pamoja na lawama hizo walieleza kusikitishwa na matamshi yaliyotolewa na Hamad , ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, kuwa Wazanzibari wote wanataka Muungano wa mkataba.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamadu Shaka, alisema jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi kuu za jumuiya hiyo huko mjini Unguja.
"Asijikweze na kutafuta sifa asizokuwa nazo, hana ubavu wala sifa halisi ya kuisemea Zanzibar, mwenye madaraka na mamlaka hayo kisheria na kikatiba ni Rais Dk Ali Mohamed Shein, Hamad akae chonjo,yeye ni mshauri wa Rais", alisema Shaka.
Alisema kitendo chake cha kuhutubia mkutano wa hadhara na kushindwa kujibu hoja zilizoelezwa na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kupinga kwake mfumo wa Muungano wa serikali tatu na kutamka Wazanzibari wote wanataka mfumo wa Muungano wa serikali ya mkataba ni uongo na uzushi usiomjengea taadhima kiongozi huyo.
Shaka alihoji Zanzibar tokea mwaka 1992 ina vyama vingi vya siasa , itikadi tofauti na kila chama kina sera zake na kuhoji Maalim Seif amepata wapi idhini ya kuwasemea Wazanzibari kama wanaunga mkono Muungano wa mkataba na si serikali mbili.
Alieleza haipendekezi kwa umri na makamo alionayo Maalim Seif kusimama hadharani na kuzua huku ameshindwa kujibu mapigo na kujenga hoja alizozianzisha Rais Kikwete akijaribu kuwajengea nadharia isiyo na tija wanachama wake kwa kutaka Muungano wa mkataba ambao haupo na hautatokea.
Shaka alieleza kuwa, ikiwa Hamad anataka Muungano wa mkataba angeyajengea nguvu ya hoja madai yake na kuonyesha faida na tija zake kama alivyotaja kasoro, hitilafu na hatari za serikali tatu kama Rais Kikwete alivyofanya.
Alisema kama Rais Kikwete alionyesha hofu hiyo na kusema mfumo wa serikali mbili una nafasi kubwa ya kuleta utatuzi, akiikosoa rasimu ya Jaji Joseph Warioba kitakwimu na kutaja vifungu vya katiba na baadhi ya ibara zinazohitaji kuangaliwa kwa umakini. Alichotakiwa ajibu kwa nguvu hoja si kusema Rais Kikwete ameuvuruga mchakato wa kupatikana katiba mpya.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI