JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA NISHATI NA MADINI | |||
TAARIFA KWA UMMA
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI PROF. SOSPETER MUHONGO KUWA MGENI RASMI SIKU YA WANATAALUMA UJERUMANI
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo atakuwa mgeni rasmi katika siku ya wanataaluma itakayofanyika Aprili 26, mwaka huu katika mji wa Berlin, Ujerumani ambapo atazungumzia fursa za uwekezaji Tanzania hususan katika sekta ya mafuta na gesi.
Profesa Muhongo atatoa mada hiyo ya fursa za uwekezaji nchini ikiwa ni moja ya shughuli zilizopangwa kufanyika katika siku mbili za kongamano la uwekezaji litakalofanyika katika mji wa Berlin, nchini humo mnamo tarehe 25 na 26 Aprili mwaka huu.
Kongamano hilo la uwekezaji limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ikiwa ni njia mojawapo ya kusheherekea Jubilee ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo makampuni mbalimbali kutoka Tanzania yanatarajia kuonesha shughuli zinazolenga katika kuonesha fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Mada nyingine zitakazowasilishwa katika siku mbili za kongamano la Uwekezaji Ujerumani ni pamoja na mahusiano baina ya Ujerumani na Tanzania na hatma ya majengo ya kihistoria Tanzania.
Kongamano hilo la siku mbili litaenda sambamba na maonesho ambapo watendaji wa Wizara na Taasisi watapata fursa ya kuelezea fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta sekta ya Nishati na Madini ikiwemo umeme, gesi asilia na mafuta, nishati jadidifu na kutoa maelezo kuhusu ramani zinazoonyesha madini yanayopatikana nchini.
Imetolewa;
BADRA MASOUD
MSEMAJI WA WIZARA
22/4/2014