KADIRI siku zinavyokwenda kumekuwapo na ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyochangia kuleta mabadiliko katika jamii. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa hasi au chanya kutegemea na aina ya bidhaa iliyogunduliwa na matumizi yake. Zipo bidhaa zinazoonekana kuwa na matokeo ya haraka na mazuri baada ya kutumika, lakini wakati huo huo kuwa na madhara kiafya kwa mtumiaji.
Nchi nyingi zinazoendelea hasa zilizopo barani Afrika ikiwamo Tanzania zimekuwa ndizo waathirika wakubwa wa bidhaa zinaotajwa kuwa na madhara huku vijana wakiwa ndiyo kundi kubwa linaloathirika. Sababu za kundi hilo kuathirika zaidi ni kutaka kwenda na wakati kwa kujaribu kutumia kila bidhaa zinazotoka nje ya nchi bila kujua madhara yake.
Miongoni mwa bidhaa hizo ni nguo za ndani zilizoundwa maalumu kwa ajili ya kupunguza unene, pia kutengeneza umbile la mvaaji katika mwonekano wenye mvuto aupendao. Nguo hizo zimetengenezwa kwa mtindo wa mbano, (Skin tight)ambapo ikivaliwa hubana eneo la tumboni hadi kwenye mapaja na hufanya kazi ya kupunguza unene, zikiufanya mwili kuwa mwembamba kulingana na nguo husika ilivyo.
Licha ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kusaidia kwa kiasi kikubwa watu wengi kupunguza miili yao, utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa nguo hizo za ndani huchangia kwa kiwango kikubwa uwezekano wa mvaaji kupata matatizo ya kiafya.
Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa nchini Uingereza, unaonyesha kuwa uvaaji wa nguo hizo unaweza kumfanya mvaaji kupata maradhi ya mgongo, saratani na kiwango kikubwa cha asidi mwilini.
Mmoja wa wataalamu wa afya katika Hospitali ya The London Clinic, Dk Johnson Wilson, anasema kubana kwa nguo hizo katika eneo la tumbo huzuia mzunguko wa asidi inayozalishwa ndani ya mwili na kuisababisha kupanda juu, badala ya kushuka chini.
Anasema kuwa hali hiyo inatokana na msukomo unaotokea kwenye tumbo, hivyo kusababisha mlundikano wa asidi ndani ya mwili ambayo hupaswa kutoka baada ya kuzalishwa.
“Nguo hii inapovaliwa inatenganisha eneo la kifuani na tumbo, hivyo asidi inayozalishwa inashindwa kushuka chini na matokeo yake inashia kwenya usawa wa matiti na kurudi kwenye mrija unaopitisha chakula,”anasema DkWilson.
Kuhusu hatari ya saratani, Dk Wilson anasema kuwa kulundikana kwa asidi katika mrija wa chakula, kunamweka mhusika katika hatari ya kupata saratani ya koo na kinywa.
Anasema kwamba licha ya kuwa siyo watu wengi walioathirika na uvaaji wa nguo hizo, lakini matokea yake huonekana baada ya muda mrefu kutokana muda ambao mhusika atavaa nguo hizo.
“Hatari ipo zaidi kwa wanaovaa nguo hizi mara kwa mara, madhara yake hayawezi kuonekana kwa haraka zaidi, lakini kiafya kuna hatari ya kutengeneza saratani ya koo kutokana na kuzuia asidi na kusababishia irudi na kulundikana kwenye mrija unaosafirisha chakula,”anaonya.
Pamoja na hatari hiyo uvaaji wa nguo hizoi pia unachangia kusababisha ugonjwa wa ngozi unaotokana na mwili kubanwa kupita kiasi, hivyo hewa kushindwa kupita.
Dk Wilson anafafanua kuwa ikifikia hatua hiyo, kuna uwezekano wa kutengeneza mazingira ya bakteria na fangasi kujificha kwenye mwili hivyo kusababisha mvaaji kupata maradhi ya ngozi yaliyo magumu kutibika.
Mtaalamu wa ngozi Dk Sam Bunting anasema, kubanwa kwa ngozi pamoja na joto linalosababishwa na msuguano, vinachangia kuleta madhara makubwa katika mwili wa binadamu.
“Hali hii inasababisha ugonjwa unaofahamika kwa jina la kitaalamu kama Intertirgo, ambao huwatokea watu wanaovaa nguo maalumu za kubana kwa ajili ya kutengeneza maumbile,”anasema.
Nguo hizo pia huchangia kuifanya misuli ya tumbo kuwa dhaifu, kutokana na kubanwa muda mwingi, hata inapoachwa huru inashindwa kuwa na nguvu yake ya kawaida.
“Kwa asili misuli ya tumbo haina nguvu na unapoibana kwa muda mrefu unaisababishia kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi, hivyo hulegea na kuwa dhaifu zaidi hata inapofunguliwa au kutolewa nguo inayobana,”anasema.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa misuli Dk Robert Shanks anasema kuwa nguo hizo zinachangia pia kusababisha maumivu ya mgongo kwa mvaaji. Anasema nguo hiyo inapovaliwa, kunakuwapo na ugumu kwa viungo vya mgongo kujongea kwa urahisi, hivyo kusababisha maumivu ya mgongo mara kwa mara.
“Viungo na mifupa iliyopo kwenye mgongo inapaswa kujongea, lakini kuibana kupita kiasi kutasababisha kushindikana kwa hali hiyo hivyo mvaaji lazima atakumbana na maumivu ya mgongo mara kwa mara”
Pamoja na madhara hayo, nguo hizi pia huweza kusababisha kizuizi katika mzunguko wa damu kwani mishipa inayotakiwa kufanyakazi hiyo inashindwa, kutokana na maeneo ya tumbo hadi kwenye nyonga yanakuwa yamebanwa.
“Ni vigumu mzunguko wa damu kufanyika vizuri katika maeneo yaliyobanwa kupita kiasi; ni wazi kuwa nguo hizi siyo rafiki, huifanya damu isizunguke inavyopaswa,”anasema Dk Shanks na kuongeza:
“Ikifikia hatua hiyo, kuna dalili mvaaji kuweza kupata maimivu ya miguu kwa kuwa mishipa ya damu iliyopo katika maeneo hayo inashindwa kufanya kazi yake vizuri.”
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya ngozi nchini Tanzania, Dk Isack Maro, anasema kuwa madhara yanayotokana na uvaaji huo siyo makubwa ikilinganishwa na ripoti ya utafiti unavyoeleza.
“Inawezekana kukawapo uwezekeno wa kupata maradhi ya ngozi kutokana na mwili kubanwa kwa muda mrefu, hivyo jasho kushindwa kutoka na kutengeneza mazingira ya fangasi,”anasema Dk Maro na kuongeza:
“Madhara yapo, lakini siyo kwa ukubwa huo. Inawezekana kuwakumba watu wachache mno kati ya wengi, lakini sidhani kama yanaweza kuwa kwa ukubwa huo.”