Kwa mujibu wa chanzo, ndugu huyo alikabidhiwa mshiko huo kiasi cha shilingi milioni mbili za Kibongo ambapo aliaminika kwamba baada ya kutua Nairobi, Kenya ambako mwili wa marehemu ulipelekwa kwa mazishi kutoka Bongo, angezikabidhi kwa familia, hasa baba na mama wa marehemu. “Yule jamaa amefika Kenya na hakukabidhi pesa. Wengi waliamini kwamba angezitoa baada ya kumzika marehemu kule kijijini Siaya, lakini baada ya mazishi tu akachomoka na kurudi Nairobi.
“Mbaya zaidi amezima simu, kwa hiyo hayupo hewani. Kuna uwezekano amerejea Dar es Salaam kwa kuogopa msala wa familia,” kilisema chanzo hicho.
Kikaongeza: “Awali wakati msiba upo Dar, kuna mtu alimpa shilingi milioni mbili akampe mama wa marehemu Kenya. Pia kuna michango mingine iliyotolewa pale Leaders Club (Kinondoni) akakabidhiwa yeye. Na kuna pesa ya kusafiria mtoto mmoja pia akapewa.
“Sasa baada ya kuzika tu, yule mtu aliyetoa shilingi milioni mbili akapiga simu kwamba na yeye anakwenda msibani, ndiyo jamaa akaaga haraka na kuondoka.
Yule alipofika akamuuliza mama wa marehemu kama alipewa shilingi milioni mbili, akasema hajapewa, kumbe jamaa aliondoka haraka kwa sababu alijua kitanuka.”
George Tyson alifariki dunia Mei 30, mwaka huu kwa ajali ya gari akitokea Dodoma kuelekea Dar. Alizikwa Juni 14, 2014 kwenye Kijiji cha Siaya, Kisumu, Kenya. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.