Shakoor Jongo na Musa Mateja
UNAWEZA kusema ni majanga juu ya majanga yanazidi kumkumba modo wa Bongo, Jacqueline Patrick ‘Jack’ baada ya wiki iliyopita kushindwa kupanda kortini kufuatia kutetereka kwa afya yake bila kufafanuliwa.
Mbali na kuwa na afya tete, pia Jack anadaiwa kulalamikia haki za msingi za kibinadamu ambazo anazikosa mahabusu kwa kuishi maisha kama ya mtu aliye kifungoni.
Akizungumza na Amani juzi jijini Dar, mtu anayejitolea kumpa msaada na kumtembelea Jack mahabusu, Macau, China alikoshikiliwa, Matilda alisema Jack anaumia kwa kupewa maisha kama tayari amehukumiwa, anaona bora hukumu yake ipite ajue moja.
“Kiukweli Jack anaumwa, alishindwa hata kwenda mahamani, mbaya zaidi hata wakili wake naye hakutokea siku hiyo.
“Halafu kule mahabusu anafanyishwa kazi ngumu ambazo hastahili kama mahabusu na amesema hata watu wake wa karibu ambao anaamini kwa kipindi hiki wangekuwa wanampa faraja hawaoni, anatamani angekamatiwa Bongo labda kuna watu wanapenda kwenda kumtembelea kule Macau lakini hawana uwezo.
“Wabongo wengi ambao wako Macau kwa ajili ya sanaa ya sarakasi ndiyo kidogo wanakwenda kumtembelea siku mojamoja,” alisema Matilda.
Juni 20, mwaka huu, Amani lilizungumza na Mbongo Fleva anayedaiwa ni mtu wa karibu na Jack, Juma Khalid ‘Jux’ na kumuuliza kwa nini hajawahi kwenda kumtembelea ‘bebi’ wake mahabusu kama wanavyofanya Wabongo ambao wako Macau, akajibu:
“Sipendi kusikia ishu yoyote inayomuhusu Jack kwani nina mambo mengi ya kuongelea na si ishu za Jack kila kukicha.
“Kwa kipindi hiki sitahitaji mtu aniulize ishu za Jack, zinanitibua sana na kama kuongelewa zimeshaongelewa hivyo sioni kipya.”
Hii ni mara ya tatu kwa Jack kupanda mahakamani, mara ya kwanza ilikuwa Aprili 10, mwaka huu kosa likiwa kukutwa na madawa ya kulevya tumboni aina ya heroin kete 57 au kilo 1.1 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 223. Mara ya pili ilikuwa Mei 23, mwaka huu.
GPL