NIkama jina la wimbo wake mpya wa Mdogo Mdogo ambao ndani yake kuna kikorombwezo ‘mwendawazimu kaingiaje’, ndiyo hali iliyotokea kwenye futari ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alipofuturisha nyumbani kwake ambapo pombe zilitibua shughuli nzima.
Pamoja na kufuturisha, pia Diamond alimwandalia pati mama yake mzazi, Sanura Kassim a.k.a Sandra aliyekuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa.
WAALIKWA WATAZAMANA
Katika tukio hilo lililojiri nyumbani kwa staa huyo maeneo ya Sinza-Mori jijini Dar mapema wiki hii, wageni waalikwa walijikuta wakitazamana na kuhoji uhalali wa chupa za pombe kuwepo ndani katika sehemu ambayo walitakiwa kufanyia dua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya wanahabari wetu, baadhi ya wageni waalikwa wakiwemo maustadhi walioshangazwa na jambo hilo, walihoji kuwa kulikuwa na ulazima gani au kilishindikana nini wahusika kuziondoa pombe hizo halafu wazirudishe baadaye.
Pombe zilizonaswa.
“Unajua huu ni mwezi wa imani zaidi, sasa linapotokea suala la ibada kama hili la kufuturisha basi kuna vitu vingine unatakiwa uvifiche ikiwezekana uachane navyo kabisa.
“Sioni sababu ya zile pombe kuachwa pale sebuleni kila aliyeingia ndani kula keki anakutana nazo uso kwa uso,” alisikika akilalama mmoja wa waumini wa Dini ya Kiislamu walioalikwa.
POMBE ZAONDOLEWA
Hata hivyo, pombe hizo kali ziliondolewa mahali hapo mara moja kisha shughuli ikaendelea.
SHAMPEINI YA WEMA YATILIWA SHAKA
Katika kuendelea kuweka walakini, muumini mwingine alikwenda mbali zaidi na kuitilia shaka shampeini iliyofunguliwa kuwa ni nani aliichunguza kama ilikuwa na kilevi au la!.
Maustadhi wakielekea kwenye futari.
“Wakati shampeini inaletwa niliona, aliileta kijana mmoja namjua kwa jina la James ambaye ndiye aliyempatia Babu Tale (meneja wa Diamond), naye akampatia Wema Sepetu (laazizi wa Diamond).
“Sidhani kama walikuwa na muda wa kusoma kama ina kilevi au la ndiyo maana baada ya Wema kuifungua watu waliikataa wakidhani ina kilevi hivyo ikamdodea mrembo huyo kwani ilidaiwa kama ilikuwa na kilevi ni jambo baya kwa mwezi mtukufu.
WAINYWA WATATU
“Walioinywa ni watatu tu, Wema, mama Diamond na dada yake Diamond, Esma Platnumz,” alisema mmoja wa waumini hao akitoa hoja juu ya kuitilia shaka shampeini hiyo ambayo waandishi wetu hawakupata nafasi ya kusoma maelezo yake.
Wageni waalikwa wakipata futari.
MSIKIE BABU TALE
Baada ya kupata maelezo hayo, Ijumaa lilijaribu kuhoji kwa wahusika ambapo Meneja wa Diamond, Babu Tale alisema kuwa licha ya kutokaguliwa kwa Shampeini lakini haikuwa na kilevi.
“Shampeini haikuwa na kilevi, lakini kuhusu suala la chupa za pombe pale sebuleni, ule ulikuwa ni urembo tu ambao upo siku zote.
“Hata mama Diamond akitaka kuswali huwa anasogeza meza na kufanya ibada yake ya swala, zile chupa zinakuwa zipo palepale ila kwa Wabongo siku zote wapo kwa ajili ya kuwakatisha watu tamaa tu.“Zile chupa huwa zipo kila siku zimekaa tu kama nilivyosema kuwa ni urembo,” alisema Babu Tale.
Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
DIAMOND HAKUWEPO
Katika shughuli hiyo, pamoja na kwamba alikuwa nchini Marekani, Diamond alimzawadia mama yake gari aina ya Toyota Lexus Harrier lililogharimu Sh. milioni 38.1 alilokabidhiwa na Babu Tale.