Neymar
BELO HORIZONTE, BRAZIL
KOCHA Mkuu wa Brazil, Luiz Felipe Scolari amesema hata Neymar angekuwapo uwanjani asingesaidia kuwanusuru na kichapo cha mabao 7-1 walichopata kutoka kwa Ujerumani kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia Jumanne iliyopita, lakini kauli hiyo imemkera wakala wa staa huyo wa Barcelona.
Wakati wengi wakiamini kwamba uwepo wa Neymar na Thiago Silva ungekuwa na faida kwa Brazil na Ujerumani wasingetamba kwenye mchezo huo, Scolari alikuwa na maoni tofauti na kudai kwamba mabeki wake walicheza hovyo.
Baada ya hilo, wakala wa Neymar, Wagner Ribeiro, amemshukia kocha Scolari na kudai kwamba kocha huyo wa Brazil ni mzigo.Wakati Wabrazili wakiwa kwenye majonzi makubwa kwa kipigo hicho cha maana, Riberio alitumia ukurasa wake wa Twitter kumshambulia kwa maneno makali kocha Felipe na kudai hana hadhi ya kuwa kocha wa timu hiyo kwa sababu ni mbahatishaji.
"Kwanza alikuwa kocha wa Ureno na hakutwaa chochote," aliandika Riberio kwenye ukurasa wake wa Twitter.
"Mbili alikwenda Chelsea na kuishia kufukuzwa tu. Tatu alikwenda kuwa kocha wa Uzbekistan. Nne alirudi Brazil na kuwa kocha wa timu kubwa (Palmeiras) na kuwashusha daraja hadi la pili.
"Tano alipoondoka kwenye klabu hiyo siku 56 kabla ya ligi ya Brazil (Brasileirao) timu ilikwepa kushuka daraja. Sita hana hadhi, mjinga na mpuuzi kabisa kwa sababu ana mambo ya kizamani."