Stori: Shakoor Jongo
Rapa maarufu Bongo, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ ameibuka na kueleza kwamba alikuwa akitumia madawa ya kulevya kwa muda mrefu lakini sasa ameamua kuacha baada ya kubaini kuna madhara makubwa.
Akizungumza kupitia Kipindi cha XXL cha Clouds Radio juzikati, Chid Benz alisema kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kushtukia kuwa alikoingia siko ndipo alikwenda kwenye matatibu nchini Kenya na hatimaye kufanikiwa kujitoa kwenye orodha ya mastaa wanaobwia kilevi hicho.
“Nilimwambia mama yangu kuwa lazima nitibiwe, nimefanya hivyo bila kwenda ‘rehab’ wala kunywa dawa, sasa niko fresh, niko healthy (nina afya), nakula vizuri, nafikiria vizuri na sasa nimetulia,” alisema Chid Benz na kuongeza:
Nilianza kutumia unga miaka mingi iliyopita lakini ilikuwa ni vigumu watu kujua kwa kuwa nilikuwa nakula vizuri, nafanya mazoezi, naoga kwa hiyo nilipokuwa nikitumia yalikuwa hayanitibui ila yananijaza tu chuki na ule unomanoma.”
Gazeti hili linampongeza Chid Benz kwa uamuzi huo na kuwataka wengine waige mfano wake.
Chanzo: Global Publishers