Mganga aliyejitambulisha kumtoa na kumngárisha msanii wa bongo flava Nassib Abdul Diamond,Dr Yahya ameapa kabla hajafa lazima haki yake ipatikane na msanii huyo atafulia na kurudi alikotoka kwasababu amedharau maagano aliyoyaweka kwake kabla hajatoka.
Dr Yahya mwezi February mwaka huu alisema kuwa Diamond amedharau maagano aliyokwenda kuweka kwake ili apate neema na mafanikio ambayo aliyapata baada ya maagano hayo.
Mganga huyo anasema kuwa baada ya Diamond kuleta dharau alianza kumshusha kutoka alipokuwa na tayari anasema msanii huyo ameanza kushuka kwakuwa kwasasa kwenye show zake halipwi milioni 10 kama ilivyokuwa zamani lakini pia show zake za Dar Es Salaam nazo haziingizi watu wengi kama zamani na sasa show anazokwenda kupiga ni za mikoani kama Tabora ambako pia hajazi watu zaidi ya kupigwa mawe na mayai viza.
Akizungumza na Times fm kipindi cha Hatua Tatu Mganga huyo ameapa kwa jina la Mwenyezi Mungu akisema hatakufa kabla ya haki yake haijapatikana na haki hiyo si pesa isipokuwa ni kutimia kwa yale anayoyaomba kupitia dua na kazi yake ya uganga kumshusha msanii huyo na kurudi alipotoka ambako alikuwa anampatia mpaka nauli.
Dr Yahya ameendelea kufunguka kuwa wimbo wa MY NUMBER ONE umefanywa kwa gharama kubwa zinazofikia milioni 50 lakini hawezi kurudisha gharama hizo kwakuwa utaendelea kuwa mzuri masikioni lakini hautamlipa na hiyo ni ishara ya kuanza kushuka kama alivyosema.
Akaenda mbali zaidi akisema kama asingejitokeza hadharana kusema hilo la Diamond kukiuka maagano kuna wasanii saba wangefariki lakini kwakuwa alijitokeza hadharani wasanii hao wamepona na wanaendelea kuwepo kulingana na maagano hayo.
Anasema kuna maagano mengi ambayo Diamond aliweka na kama akiyasema yote inawezekana watu wasimpe mkono msanii huyo na makubwa zaidi kumpata.
Diamond kwa upande wake alimkana mganga huyo akisema hakuna kitu kama hicho na kama kuna ukweli yuko tayari kushushwa alikotoka.