Kifaru cha kivita cha JWTZ kikifanya matayarisho ya mwisho kwa ajili ya maadhimisho ya kilele cha sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Gari za Polisi zinazotumika wakati wa kuzuia vurugu katika maeneo mbali mbali nchini zikipita mbele ya jukwaa kuu wakati zikiwa katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar zitakazofanyika Jan 12 katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakionyesha ukakamavu wao wakati wa maandalizi ya mwisho ya maadhimisho ya kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { jwtz } wakionyesha ustadi wao wakati wa mazoezi ya mwisho kwa ajili ya sherehe za kutimia nusu karne ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Askari wastaafu wa Jeshi la Ukombozi la Unguja (JLU) ambalo linatarajiwa kuonyesha vitu vyao wakati wa kilele cha maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baadhi ya wanafunzi wa halaiki wa skuli mbali mbali za Zanzibar na Tanzania Bara wakiwa katika mazoezi ya mwisho kujiandaa na sherehe za mapinduzi.Picha na Hassan Issa-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
----
Na Othman Khamis Ame
Jumapili ya Januari 12 mwaka 2014 Watanzania wanatarajiwa kujumuika katika maadhimisho ya kilele cha kutimia miaka 50 sawa na nusu karne ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika katika tatan za uwanja wa Amani Mjini Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammd Sheni atalihutubia Taifa uwanjani hapo hotuba itakayo rushwa na kusikika moja kwa moja katika vyombo mbani mbali vya Habari hapa Nchini.
Matayarisho ya mwisho ya gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vya majeshi yote ya ulinzi Nchini Tanzania yamekamilika vyema katika uwanja wa amani Mjini Zanzibar .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, maafisa wa vikosi vya ulinzi pamoja na baadhi ya wananachi walishuhudia mazoezi hayo ya mwisho yanyiyoonekana kufana sana.
Matayarisho hayo yalikwenda sambamba na mazoezi ya ndege za Kivita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } ambazo zilikuwa zikipita na kuonyesha ustadi wake ndani ya eneo la mji wa Zanzibar kushajiisha umuhimu wa maadhimisho hayo ya kihistoria.
Kazi pevu na nzito iliyowaacha midomo wazi Makamanda, Viongozi na Mwenyekiti mwenyewe wa Kamati ya Maadhimisho ya kitaifa Balozi Seif ilifanywa na vijeba wa Jeshi la Wananchi wa Taznzania { JWTZ } wa Kikosi maalum cha Makomandoo.
Ukafikia wakati wa onyesho maalum la magari ya kivita ya jeshi la wananchi wa Tanzania yaliyoongozwa na gari maalum zilizobeba baadhi ya silaha za kivita kitendo kinachoonyesha umakini na umadhubuti wa Jeshi hilo.
Onyesho hilo lilifuatiwa na lile la vikosi maalum vya askari polisi vinavyohusika na mapambano dhidi ya wahalifu na wavunjaji amani ya Nchi ambavyo baadhi ya wakati hulazimika kutumia mbwa , farasi na hata gari za maji katika njia ya kurejesha hali ya amani hapa nchini.
Burdani ya aina yake ikatokea ndani ya viwanja vya amani pale askari wastaafu wa lililokuwa jeshi la ukombozi la Unguja { JLU } walipofanya vitu vyao wakionyesha umahiri wao kwamba bado damu ya jeshi inaendelea kuwachemka ndani ya miili yao.
Matayarisho hayo ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yakahitimishwa na watoto wa halaiki wapatao 2236 kutoka skuli mbali mbali za Zanzibar na Tanzania Bara.
Watoto hao waliweza kuufunika uwanja huo vitendo vilivyowafanya Viongozi na makamanda walioshuhudia maajabu ya watoto hao yaliyoambatana pia na sarakasi wasitulie katika viti vyao