THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com Fax: 255-22-2113425 | PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA UMMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Januari 18, 2014, amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wapya wa mikoa mitano na kuhamisha makatibu tawala wengine na Wakurugenzi wa Majiji nchini.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa jioni ya leo, Ikulu, Dar Es Salaam inasema kuwa uteuzi na uhamisho huo unaanza leo hii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makatibu Tawala wapya ni Ndugu Wamoja A. Dickolangwa ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa ambako alikuwa Kaimu Katibu Tawala; Ndugu Abdallah D. Chikota ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya Newala na Ndugu Symthies E. Pangisa ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa. Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Pangisa alikuwa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Ndugu Alfred C. Luanda ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara. Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Ndugu Jackson L. Saitabau ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe. Kabla ya hapo, alikuwa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Arusha.
Taarifa hiyo iliwataja waliohamishwa kuwa ni Ndugu Beatha Swai aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na sasa anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Sipora J. Liana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Benedict Ole Kuyan ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga anahamishiwa Mkoa wa Mara na Ndugu Salum M.Chima ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa anahamishiwa Mkoa wa Tanga.
Wengine waliohamishwa ni Ndugu Mgeni Baruani ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe anahamishiwa Mkoa wa Pwani; Ndugu Juma R. Iddi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya anahamishiwa Jiji la Arusha kama Mkurugenzi; Eng. Omari Chambo ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi anahamishiwa Mkoa wa Manyara kama Katibu Tawala wa Mkoa huo na Dkt. John Ndunguru aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi anahamishiwa Mkoa wa Kigoma kama Katibu Tawala wa Mkoa huo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Januari, 2014