MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amemtaja Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali kuwa ni adui namba moja wa klabu hiyo.
Manji alisema hayo jana wakati wa mkutano mkuu wa wanachama wa Yanga uliofanyika kwenye ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam.
Alisema Akilimali ni chanzo cha migogoro ya mara kwa mara ndani ya klabu hiyo kongwe nchini na amekuwa akimpa wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yake.
"Huyu mzee wakati naingia Yanga, alinipokea na alinifanyia kampeni nishinde, cha ajabu ananitukanisha katika vyombo vya habari, ananivua nguo, ananifanya nishindwe kutekeleza wajibu wangu ipasavyo,"alisema Manji.
Aliongeza kuwa, Akilimali amekuwa akiingilia mambo ya Yanga kama kwamba ni msemaji mkuu na mwenye mamlaka katika klabu hiyo, hali ambayo imeleta mgawanyiko.
Manji alisema Akilimali anavunja katiba ya Yanga kwa kuwa, haitambui kuwepo kwa Baraza la Wazee, isipokuwa viongozi wamekubali uwepo wake kutokana na busara zao katika ustawi wa klabu.
Hata hivyo,baada ya kumpasulia Akilimali ukweli huo, Manji aliamua kumfuata, akazungumza naye kwa sekunde kadhaa na kisha kumkumbatia.
Katika hatua nyingine, Manji amewaeleza wanachama wa Yanga kwamba hana mpango wa kuwania tena uongozi wa klabu hiyo katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Alisema uamuzi wake wa kuwania uenyekiti wa Yanga ulilenga kuwatuliza wanachama wa klabu hiyo baada ya kuchapwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya mwisho ya ligi kuu.
"Tayari amani imerejea, sitaki kugombea tena uongozi na sitaki suala hili lijadiliwe tena,"alisema Manji. You mig