Miongoni mwa wanamuziki wa Bara la Afrika waliowahi kuandika historia mbili tofauti za uhusiano ni mwanamuziki M’bilia Bell.
Mwanamama huyu ambaye jina lake kamili ni Marikirala Mboyo M’bilia Bell, alizaliwa mwaka 1959 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alianza muziki alipokuwa na umri wa miaka 17, wakati huo akiwa na mkongwe hayati Abeti Massekini mwaka 1976.
Historia zilizoandikwa na M’bilia Bell ni pamoja na kukataa kuolewa na Waziri katika Serikali ya nchi ya Gabon iliyopo Afrika ya Kati, nyingine ni kufunga ndoa akiwa ndani ya ndege angani na aliyekuwa mwanamuziki mahiri wa Kongo hayati Tabu Ley Rochereau.
Mbilia Bell alijifunza muziki baada ya kuvutiwa na sauti ya babu yake aliyekuwa bingwa wa kuimba, wakati bibi yake alikuwa mcheza ngoma maarufu kijijini kwao na vijiji jirani.
Katika maisha yake, M’bilia aliwahi kusema kwamba, pamoja na kuvutiwa na uimbaji wa babu na bibi yake, alipata hamu ya kuingia rasmi kwenye muziki baada ya kumwona mwanamuziki nyota kutoka nchini Togo, Bela Bello.
Alimwona Bello kupitia televisheni akifanya onyesho katika Mji wa Kinshasa, huko DRC.Tangu hapo aliweka nadhiri ya kujitahidi ili awe kama Bello na hata alipopata taarifa za kifo chake, alimlilia kwa zaidi ya wiki moja.
Mbilia alikuwa akipenda kuangalia wanamuziki walipokuwa kwenye shoo mbalimbali kupitia runinga ndipo siku moja akatokea kuvutiwa tena na mwanamuziki AbÈti Massekini.
Baadaye M’bilia Bell aliamua kumwandikia barua AbE’ti akiomba kujiunga na bendi yake na alikubaliwa bila kipingamizi ndipo alianza kujifunza kuimba akiwa na mkongwe huyo kwa miaka minne.
Alipokuwa na AbÈti, alifanya mawasiliano na mwanamuziki mkongwe Sam Mangwana na kufanikiwa kujiunga naye, ingawa baada ya miaka miwili yaani mwaka 1981, alijiunga na gwiji la muziki wa Afrika Tabu Ley.
Kabla ya kujiunga na bendi hiyo aliwahi kumwona akifanyiwa mahojiano na kituo cha televisheni, hivyo kutamani kufanya naye kazi na Tabu Ley bila hiyana alikubali na kumwahidi kumfanyia makubwa.
Alijiunga na Bendi ya Afrisa Internationale na kuiongezea umaarufu kutokana na ucheshi, uchezaji wake na maungo yake yaliyojengeka Kiafrika hata bendi hiyo ikawa maarufu ikaongezeka mapato yake.
Baada ya kuwa kwenye bendi hiyo M’bilia na Tabu Ley walianzisha uhusiano wa kimapenzi na baadaye kufunga ndoa ya kifahari wakiwa ndani ya ndege angani.
Katika ndoa yao walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Melodie Tabu, ambaye sasa anasoma katika Jiji la Paris nchini Ufaransa.
Mwaka 1982 mwanamke huyu aliachia kibao kiitwacho Mpeve ya Longo, kikisimulia kisa cha mwanamke aliyetelekezwa na mumewe na kuachiwa watoto amlee peke yake. Kibao hicho kiligusa hisia na kuwa simulizi kila kona za Jiji la Kinshasa.
Wakiwa na Tabu Ley, pamoja na kuimba nyimbo nyingi, wimbo uliowapatia umaarufu ni “Mobali na Ngai Wana”, jina hilo likiwa na maana ‘Huyu ni mume wangu’.
M’bilia Bell aliwahi kufika Tanzania akifuatana na mumewe Tabu Ley ambaye sasa ni marehemu, wakiwa na kundi zima la Afrisa Internationale.
Ndoa yao iliiingia dosari baada ya kuongezwa mwanamuziki wa kike ‘Faya Tess’ ambaye jina lake halisi ni Kishila Ngoyi. Ujio wa Faya Tess ulimfanya M’bilia kuamua kuiacha bendi hiyo na kwenda Paris, ambako alikutana na mwanamuziki wa Sokous, mpiga gitaa Rigo Star Bamundele mwaka 1983.
Sababu kubwa za kuondoka kwake ni kile kilichoelezwa kuwa wivu wa mapenzi baina ya wanandoa hao, ulioingiliwa na Faya Tess.
Marikirala Mboyo (M’bilia) aliwahi kueleza kuwa haikuwa kazi rahisi kukubalika kuwa mwanamuziki mwanamke wa kimataifa katika maisha yake yote ya kazi za muziki.
“Watu wengi hawakuwa wakimwamini na kuichukulia kazi yake kwamba haitakuwa endelevu,” alisema M’bilia.
Mwanamke huyo ameitaja sababu ya kuwa na mwonekano mzuri licha ya kuwa na umri mkubwa kuwa ni kutokana na kufanya mazoezi.
Ratiba yake huamka kila siku saa 12:00 asubuhi na kufanya maombi, baadaye huenda kwenye mazoenzi ya viungo na kwamba hanywi pombe wala kula nyama.
Chakula
Ratiba yake ya asubuhi ni kunywa glasi moja ya maziwa isiyokuwa na mafuta na glasi nyingine maji huwa ndiyo kifungua kinywa chake.
Baada ya hapo hutumia muda mwingi katika kuandika nyimbo zake na kuangalia sinema katika televisheni.
Nyimbo zilizompatia umaarufu ni pamoja na ‘Nakei Nairobi’, ‘Boya ye’, ‘Yamba ngay’, ‘Amour sans frantiere’ na ‘Biu Mondo’.
Nyimbo nyingine ni pamoja na zile alizoimba kwa lugha ya Kiswahili ikiwamo Nadina na Nelson Mandela.
Nyimbo nyingine alizoimba ni pamoja na Phenomene, Manzil Manzil, Mbanda na Nga, Mayaval, Eswii yo Wapi, Biu Mondo na Wende na Wende.