Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema

kuwa kamwe hatakiacha chama hicho katika uchanga wa harakati za kulikomboa taifa kama kiongozi wake wa juu.


Akihutubia katika mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima katika sehemu mbalimbali mkoani Morogoro jana,

mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa, bado atagombea nafasi ya uenyekiti kwa lengo la kuendeleza harakati za ukombozi

wa pili wa taifa hili.

Halima Mdee anguruma
Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambaye yuko katika msafara wa mwenyekiti huyo, alisema vijana wengi wanaochipukia katika

siasa kupitia chama hicho, wamelelewa na Mbowe, ambao leo wamekuwa chachu ya mabadiliko nchini.


“Ukweli ni kwamba kamanda huyu wa anga (Mbowe), ndiye ametulea vijana wengi nikiwemo mimi, tena wengine hatukuwa na ujasiri

tulionao sasa, asiwadanganye mtu, hasa sisi vijana kwamba tuliingia CHADEMA na umaarufu, hawapo hao, tumelelewa na huyo

kamanda,” alisisitiza huku akipigiwa makofi.



Bila kutaja jina, Mbowe alionya kuwa wenye fikra za kuachiwa chama hicho kikiwa katikati ya ukombozi huo

hawatapata nafasi, kwa sababu hawana nia thabiti ya kukiendeleza, bali wana nia ya kukibomoa kwa kutumiwa na

wapinzani wa CHADEMA.


“Makamanda, kumbukeni kuwa chama hiki na sisi viongozi wake tumepita katika majaribu makubwa na hata

kukoswakoswa kuuawa. Mimi nimekoswakoswa kuuawa kwa bomu huko Arusha, lakini pia kuna watu wamepoteza

maisha, wamefungwa jela, wengine wamekuwa vilema, halafu watu wengine wanatusaliti kwa kupewa visenti ili

wakivuruge chama na wanataka tuwape chama. Huu ni uendawazimu,” alisema.


Mwenyekiti huyo alisema CCM imekuwa ikifanya jitihada za kuihujumu CHADEMA kwa mbinu mbalimbali, zikiwemo za

kupandikiza migogoro, jambo ambalo limeshindwa kufanikiwa kwani Mungu ameweka mkono wake ili kisisambaratike.


“Harakati hizi tunazofanya za kuwakomboa Watanzania mjue tunahatarisha maisha yetu, tumejaribiwa kushawishiwa

ndani na nje ya Bunge ili tuwe kondoo, tumekataa. CCM wamekuja na mbinu za kupandikiza migogoro wameshindwa na

sasa wanaomba nife wakifikiri nikifa na CHADEMA itakufa. Nawaambia CHADEMA haifi kwa kuwa tumezalisha

makamanda wengi, watakiendeleza,” aliongeza Mbowe.


Akielezea kwa mara ya kwanza kwa undani zaidi kuhusu mauaji ya Arusha, mwenyekiti huyo alisema wana ushahidi wa

kutosha kwamba polisi walihusika na mauaji hayo na kuongeza kuwa waliohusika ni polisi wa kutoka mkoani Morogoro.


“Kwa mara ya kwanza niliseme hili, mauaji ya Arusha yaliyofanyika kwa kurusha bomu katika mkutano wa kampeni za

CHADEMA, yalifanywa na polisi ambao walitoka mkoani Morogoro. Ndiyo maana tunaendelea kumwambia Rais Jakaya

Kikwete aunde tume ya kimahakama ili kupata ukweli wa jambo hili,” alisema.