MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba amewataka wanawake na vijana wa Jimbo hilo kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali likiwemo shirika la Maendeleo la Bumbuli.
Akizungumza kwa niaba ya Makamba,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bakari Kavumo wakati wa uzinduzi wa kikundi cha Tumaini (VIKOBA) kilichopo kata ya Soni alihimiza uanzishwaji wa vikundi na kwamba kufanya hivyo kutawarahisishia upatikanaji mikopo na misaada kwa wahisani.
Pia Mbunge huyo alichangia shilingi 3. milioni kama mtaji wa kuendesha kikundi hicho ambacho kimezinduliwa katika jimbo lake lengo kubwa kuwakomboa wanawake na umaskini.
Alisema ni vema wananchi hao wakaanzisha vikundi maalumu ambavyo vitafahamika kisheria na hivyo kuwa njia mbadala ya kujinasua na umasikini badala ya kutegemea shughuli za mtu mmoja mmoja.
Makamba ambae pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia aliahidi kusimamia vikundi hivyo na kuhakikisha kuwa akinamama na vijana waliyojiunga wanapata mikopo kutoka Shirika hilo la Maendeleo ya Jimbo la Bumbuli (BDC).
Alisema atatekeleza hayo ikiwa ni miongoni mwa ahadi zake alizozitoa wakati wa kuomba ridhaa ya ubunge kwa wakazi wa Jimbo hilo na kwamba licha ya mikopo hiyo atahakikisha kuwa sekta zote muhimu zinapata mabadiliko huku akiwa na nia kuwakwamua wana bumbuli kiuchumi.
Shirika la Maendeleo la Bumbuli lilianzishwa rasmi mwaka juzi na Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba kwa ajili kuratibu na kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.
Taasisi ya Utoaji Mikopo ya shirika hilo, BDC-MFI imeanzishwa kama chombo cha kuziba pengo lililopo la ukosefu wa mitaji na vyombo vya utoaji mikopo kwa ajili ya wajasiriamali wa kawaida.
MWISHO