BUNGE LAKANUSHA TUHUMA ZA PAUL MAKONDA KUHUSIKA NA WIZI WA SIMU BUNGENI.
Kitengo cha ulinzi na usalama cha Bunge kimetoa taarifa ya kukanusha, tuhuma zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zikimhusisha Mbunge wa Bunge maalumu la Katiba ndugu Paul Makonda kuhusika na wizi wa simu ya Mjumbe wa Bunge la Katiba. Akitoa taarifa hiyo mbele ya Bunge maalumu la katiba, Mwenyekiti wa muda wa Bunge maalumu, Mh. Pandu Amiri Kificho alisema;
"Waheshimiwa wabunge taarifa inasomeka kama ifutavyo;
Taarifa ya upotoshaji zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Mh. Paul Makonda, anahojiwa na vyombo vya usalama vya Bunge kwa tuhuma za wizi wa simu.
(Sasa Kitengo cha usalama chetu ambacho hicho kinachotegemewa ndiyo kinamuhoji, kinatoa taarifa hii,ili kuweka wazi na kuondoa hiyo tuhuma ya upotoshaji iliyotolewa)
Mnamo tarehe 27/02/2014 kwenye vyombo vya habari hususani kwenye mitandao ya kijamii, zilitolewa taarifa kwamba Mh. Paul Makonda anashikiliwa na vyombo vya usalama vya Bunge kwa mahojiano kutokana na tuhuma za wizi wa simu ya mjumbe mwenzake ndani ya ukumbi wa Bunge. Mtoa taarifa kwenye mitandao hiyo alieleza kwamba, wakati anatoa taarifa yake Mh. Paul Makonda, alikuwa chini ya ulinzi akipekuliwa na kuhojiwa kwa tuhuma za wizi huo. Kitengo chetu kinasema ukweli ni kwamba, taarifa hiyo ni ya uongo (makofi) na yenye nia ya kumchafua Mh. Paul Makonda (makofi) pamoja na taswira mzima ya Bunge Maalumu. Mh. Paul Makonda ambaye ni mjumbe wa Bunge hili maalumu hana tuhuma yeyote inayohusiana na wizi wa kitu (makofi) chochote ndani ya maeneo ya Bunge hili maalumu, tangu ajisajiri kama mjumbe wa Bunge hili maalumu na wala hajawahi kupekuliwa na kutuhumiwa (makofi) kwa kosa lolote la aina hiyo na hivyo hashikiliwi wala haojiwi na chombo chochote cha usalama wa Bunge (makofi).
Waheshimiwa wabunge naomba niendelee kukemea, kwa mambo ya namna hii, ambayo yanachafua Mjumbe mmoja mmoja na hatimaye kuchafua Bunge hili maalumu lenye heshima kubwa (makofi). Tuwaombe wote wenye mitandao ya kijamii, lakini na vyombo vingine vya habari vyote tuache mtindo huu. Tuache mtindo huu, ni mambo ambayo yanaweza kumpa nafasi yule, ambaye anazuliwa kwa tuhuma za uongo wa aina hiyo, hata kuweza kufungua mashtaka akiona inafaa (makofi). Hii ni kwa yule atakayekuwa ametuhumiwa, lakini bado kwa kutuhumiwa mjumbe mmoja wapo, kwa taarifa za uongo za aina hii, hii inachafua heshima ya Bunge hili (makofi). Kwa hiyo, niiombe mitandao hiyo ya kijamii, niombe vyombo vya habari, Televisheni na Radio hata wale wanaoandika kwenye magazeti mbalimbali kwamba jambo hili hatutaki litokee kwa mara nyingine tena (makofi). Tujitahidi sana, tuwe tunatoa taarifa zenye ukweli ambazo zitakua na maana kwa jamii yetu ya Tanzania. Jambo hili tuachane nalo, halifai, lisituchanganye na kutuvunjia heshima zetu wajumbe lakini pia Bunge hili maalumu tukufu.
Nawashukuru sana kwa hilo" |