Kikosi cha Simba cha mwaka 1977 kilichopeleka maafa Jangwani.
Na Daniel Mbega
KATIKA mchezo wa soka kushinda ama kushindwa ni mambo ya kawaida, lakini vipo vipigo ambavyo timu hupata kiasi cha kujiuliza mara kumi kumi, kulikoni? Kama kuna kipigo ambacho kitabaki katika kumbukumbu za Yanga milele na milele ni kile cha mwaka 1977 cha magoli 6-0 kutoka kwa watani wake wa jadi, Simba, kwenye mchezo wa Ligi ya Taifa.
Kwa waliokuwepo na waliopata simulizi baadaye, Jumanne ya Julai 19, 1977 ilikuwa siku yenye majonzi makubwa kwa mashabiki wa Yanga na furaha kubwa kwa wale wa Simba, ambayo kwa ushindi huo, mbali na kujihakikishia ubingwa wa Ligi ya Taifa kwa kuwa ilibakiza mechi moja tu dhidi ya Navy (sasa KMKM) ya Zanzibar iliyokuwa ya kukamilisha ratiba, pia ilikuwa imefanikiwa baada ya miaka tisa kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-0 na Yanga mwaka 1968.
Kati ya watu waliojihisi wenye furaha kupindukia walikuwa kocha wa Simba, Dimitier Samsarov wa Bulgaria ambaye alikuwa na muda mchache tu tokea akabidhiwe timu na nahodha Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ambaye siku hiyo ‘alicheka’ na nyavu mara tatu.
Ilikuwa hadithi ya kifo cha nyani miti yote huteleza, kwani pamoja na kukuru kakara zote za Yanga, ikiwemo kubadilisha wachezaji wawili dhidi ya mmoja wa Simba, ambaye alibadilishwa kufuatia mwenzake kuumia (Martin Kikwa ndiye aliyeumia na kumpisha Abbas Dilunga), mambo yalichacha na kuvunda kwa vijana wa Jangwani waliokuwa wakipokea mashambulizi mfululizo na kubaki wakitumia ujanja wa mtego wa kuotea (offside-trick), ambao hata hivyo, haukusaidia kitu.
Mwaka huo Yanga ilikuwa haijatulia baada ya mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 uliopelekea karibu wachezaji 20 nyota kufukuzwa kwa madai ya kutokuwa wazalendo na kusababisha Yanga kupoteza taji lake la ubingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka huo. Wachezaji hao ni Gibson Sembuli, Leodgar Tenga, Sunday Manara, Boi Idd ‘Wickens’, Ally Yusuf, na wengineo ambao walikwenda kuunda timu ya Nyota Afrika ya Morogoro kabla ya kuanzisha Pan African ya Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba walifanikiwa kujipatia magoli matatu katika kipindi cha kwanza licha ya kucheza huku wakipingana na upepo katika kipindi hicho. Sentahafu wa Yanga, Selemani Jongo, ndiye aliyeonekana kuwa kikwazo pekee kwa Simba na hata yeye alilazimika ‘kukubali yaishe’ baada ya washambuliaji wajanja wa Simba kumshitukia, hivyo kumuandama kama nyuki.
Katika dakika ya pili tu mashabiki, ambao walianza kuingia uwanjani tangu saa 6.00 mchana, walishuhudia Martin Kikwa wa Simba akitolewa nje baada ya kugongana na Boniface Makomole aliyekuwa beki wa kulia wa Yanga na nafasi yake kuchukuliwa na Abbas Dilunga.
Baada ya kosa kosa nyingi kwenye goli la Yanga na takribani moja tu kwenye goli la Simba pale juhudi za mshambuliaji wa Yanga, Yanga Fadhil Bwanga zilipozimwa na golikipa wa Simba Omari Mahadhi bin Jabir, hatimaye karamu ya magoli ilianza kwa Simba kwenye dakika ya 10. Goli hilo la kwanza lilianzia katikati ya uwanja ambapo Aluu Ally wa Simba aliwakata chenga beki Charles Mwanga na kiungo Sam Kampambe na kumpasia winga wa kulia, Willy Mwaijibe, ambaye naye alitoa pasi safi kwa Jumanne Hassan ‘Masimenti’. Beki Selemani Jongo wa Yanga alitoka kuucheza mpira huo lakini Jumanne alimuwahi na kumuunganishia Abdallah Kibadeni aliyekimbia na mpira hatua chache kabla ya kuujaza wavuni huku kipa Bernard Madale akiwa hana la kufanya.
Yanga ilikukuruka baada ya goli hilo na kukaribia kusawazisha kwenye dakika ya 18 lakini shuti la nambari 8 wao, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, lililokuwa limeshawanyamazisha mashabiki wa Simba, lilipaa juu ya goli.
Hata hivyo, Yanga ilikuwa kama imejichongea, kwani golikiki iliyopigwa kunako dakika ya 20 kufuatia kosa kosa hiyo ndiyo iliyozaa goli la pili la Simba baada ya gonga za hapa na pale kumfikia Willy Mwaijibe aliyefumua shuti la chini chini ambalo katika juhudi za kuokoa, Selemani Saidi Sanga wa Yanga alijikuta akiusindikiza mpira wavuni. Zikiwa zimesalia dakika chache kuwa mapumziko, kona ya Willy Mwaijibe ilimkuta Kibadeni katika nafasi nzuri na akaujaza mpira wavuni na kuifanya Simba imalize kipindi cha kwanza ikiongoza kwa magoli 3-0. Hiyo ilikuwa dakika ya 42.
Katika kipindi cha pili, Yanga ilijitahidi kutafuta magoli ya kusawazisha lakini baada ya dakika 15 kupita wakiwa bado hawajafanikiwa kuingia kwenye eneo la goli la Simba wakiishia tu nje ya eneo la penati, kibao kiliwageukia kwa Aluu kumtangulizia pasi Jumanne aliyemzidi maarifa Jongo na kusalimiana na kipa Madale na kupachika goli la nne, na dakika 13 baadaye Aluu Ally alimpasia tena Jumanne ambaye kwa mara nyingine alimpita Jongo na kufunga goli la tano.
Yanga ilikosa kona kadhaa ilizopata. Katika dakika ya 89 Abbas Dilunga alichomoka kwenye wingi ya kushoto na kumtolea ‘chumba’ Kibadeni aliyekamilisha karamu ya magoli na kuwaacha mashabiki wa Simba wakilia kwa furaha huku wale wa Yanga wakitokwa na machozi ya simanzi. Kwa kweli kilikuwa kipigo cha kihistoria.
Mechi hiyo iliingiza jumla ya shilingi 293,664 ambazo kwa wakati huo ndiyo yalikuwa mapato makubwa zaidi kupatikana katika mechi ya ligi. Kabla ya hapo, pambano la timu hizo mwaka 1974 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ndilo lilikuwa likiongoza kwa mapato ambapo lilikuwa limeingiza shilingi 150,000.
Katika mechi hiyo, timu zilipangwa hivi:
SIMBA: Omari Mahadhi bin Jabir, Shaaban Baraza, Mohammed Kajole, Aloo Mwitu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Athumani Juma, Willy Mwaijibe, Aluu Ally, Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Abdallah Kibadeni (nahodha) na Martin Kikwa/Abbas Dilunga. Kocha: Dimiter Samsarov (Bulgaria)
YANGA: Bernard Madale, Boniface Makomole, Selemani Saidi Sanga, Charles Mwanga/Fidelis, Selemani Jongo, Sam Kampambe, Ayub Shaban/Mrisho Caraby, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, Mwinda Ramadhani ‘Maajabu’ (nahodha), Yanga Fadhil Bwanga na Shaaban Katwila.