Kahawa.
Utafiti umethibitisha kuwepo uhusiano kati ya ukosefu wa usingizi na matatizo ya kiafya kama vile ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa kisukari na saratani
KINACHOSABABISHA UKOSEFU WA USINGIZI
Ingawa msongo wa mawazo nao unatajwa kuchangia mtu kukosa usingizi, lakini mlo unaweza kuwa ndiyo sababu kubwa inayoweza kumkosesha mtu usingizi, na hasa vyakula vitano vifuatavyo:
POMBE
Unywaji wa bia moja ama mbili unaweza kukufanya upate usingizi haraka, hivyo kukufanya uamini kuwa pombe inasaidia mtu kupata usingizi haraka. Ingawa unaweza kupata usingizi haraka kwa kunywa pombe, lakini utafiti umeonesha kuwa usingizi huwa unakata usiku wa manane, au sehemu ya pili ya usingizi na kukuamsha asubuhi ukiwa mchovu.
KAHAWA
Inajulikana kwamba kahawa ndiyo chanzo kikuu cha kilevi aina ya ‘caffeine’. Inaelezwa kwamba kilevi hiki hudumu mwilini kwa muda usiopungua saa tano, hivyo kutegemeana na wakati gani umetumia kahawa, athari zake huweza kuonekana hadi usiku wakati wa kulala.
Hivyo kwa mtu mwingine, hasa mwenye matatizo ya usagaji chakula tumboni (poor metabolism), kikombe cha kahawa utakachokunywa mchana, athari zake zinaweza kuonekana hadi usiku wakati wa kulala, kwani unaweza kujikuta unapoteza usingizi wakati kahawa ulikunywa mchana au asubuhi.
Chokoleti nyeusi.
CHOKOLETI NYEUSI (Dark chocolate)
Ingawa chokoleti kwa kawaida, huwa na faida ya kuimarisha kinga ya mwili kwa kuwa na kiasi kingi cha virutubisho aina ya ‘antioxidant’, lakini pia ina kiwango kingi cha ‘caffeine’ ambacho kinaweza kuchangia ukosefu wa usingizi kama tayari unalo tatizo hilo.
VYAKULA VYENYE VIUNGO VINGI
Vyakula vilivyoungwa kwa viungo vingi vya aina mbalimbali, zikiwemo pilipili, huchangia tatizo la chakula kushindwa kusagika vizuri tumboni hali ambayo humfanya mtu kupata usingizi kwa tabu. Inaelezwa kuwa kirutubisho aina ya ‘capsaicin’ kinachopatikana ndani ya pilipili, huongeza joto la mwili na ndicho kinachochangia mtu kukosa usingizi.
VYAKULA VYENYE MAFUTA
Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pia navyo vinatajwa kuchangia ukosefu wa usingizi au usingizi wa kukatika mara kwa mara. Hivyo katika kushughulikia tatizo la kukosa usingizi usiku, huna budi kujiepusha na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, hasa vile vya kukaanga, muda mfupi kabla ya kupanda kitandani kulala.
USITUMIE VIDONGE
Wengi wenye matatizo ya kukosa usingizi hukimbilia kumeza vidonge vya usingizi. Kitendo cha kumeza vidonge vya usingizi huwa hakiondoi tatizo, bali husogeza mbele tatizo kwa kuudanganya ubongo. Zaidi wanaotumia vidonge ili kupata usingizi, huamka wakiwa wamelewa.
DONDOO ZA KUKUSAIDIA KUPATA USINGIZI
Kabla ya kulala, kunywa glasi ya maziwa moto au ya uvuguvugu. Au kula karanga au siagi ya karanga (peanut butter). Au kula zabibu kadhaa. Vyakula hivyo, ingawa vipo na vingine vingi, vinatajwa kuwa na virutubisho vinavyozalisha homoni za usingizi kwa wingi.
Aidha, kwa wenye matatizo ya kukosa usingizi kwa muda mrefu, wanashauriwa kulala kwenye chumba chenye giza kabisa, kujiepusha na kuangalia TV wakiwa wamelala kitandani, kulala mbali na simu, redio, saa na vitu vingine vyenye sumaku. Vitu hivi vimeonekana kuharibu mtiririko wa usingizi kwa njia moja au nyingine hivyo kwa mtu mwenye matatizo ya kukosa usingizi akaenavyo mbali.