"Serikali 2 na nusu suluhisho pekee la Muundo wa Muungano: Nimekuwa nikitafakari njia pekee ya kutokea endapo tuna hofu ya kupata muafaka aidha tutapata Serikali 2 ama 3, na hatima ya kumaliza mchakato huu tukiwa wamoja, nikagundua innovation ya kuwa na Bunge la Tanganyika inaweza kuwa dawa. Bunge hili litatunga sheria na litasimamia mambo yote nje ya Muungano. Hivyo, kutakuwa na vyombo vitatu vya kutunga sheria. Wajumbe wa chombo cha Tanganyika na wale wa kile cha Zanzibar watakutana kwenye Bunge la Muungano tu, ama vyombo vya Tanganyika na Zanzibar vitapaswa kuteua wajumbe wake wachache miongoni mwao ambao watawawakilisha wenzao kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo watapitisha Bajeti ya Muungano na kusimamia utendaji wa zile Wizara za Mambo ya Muungano tu. Waziri Mkuu atapaswa kupewa nguvu zaidi ndani ya Tanganyika na Rais wa Zanzibar atapaswa kupewa nguvu zaidi ndani ya Zanzibar. Nchi itabaki kuwa moja yenye dola kamili mbili (Muungano na Zanzibar). Nimetafakari sana na kuona: hivi TAMISEMI ni nini? Ipo chini ya Waziri Mkuu. Haya mawizara ya kilimo, elimu, mifugo, maji, maliasili na utalii, afya, elimu n.k. ni kwa nini yasiishie ndani ya Tanganyika tu ama Zanzibar kwa uhalisia wake kuliko kuyaficha ndani ya 'koti la Muungano' (kwa lugha ya Wazanzibari)? Wakati kiuhalisia ni mawizara ya Tanganyika tu? Ninachokoza mjadala tu, ninaamini kwa pamoja tukifikiri zaidi tunaweza kuboresha vizuri zaidi."
↧