Mapigano ya kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji katika eneo la mpaka kati ya wilaya za Kishapu mkoani Sninyanga na Igunga, mkoani Tabora yameua watu watano.
Mapigano hayo yaliyotokea Jumapili iliyopita katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu na kusababisha vifo hivyo na mtu mmoja kujeruhiwa baada ya kushambuliana kwa kutumia mikuki.
Waliouawa ni Peter Korongo Masolwa(72) Chawalwa Duke(50) Diblo Kingu(50) Mohamed msengi(40) Kende Doma(70) wakazi wa Kishapu na Igunga.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilison Nkhambaku, alisema mapigano hayo yalitokea eneo la Magogo na kwamba wafugaji wa jamii ya Kitaturu walinyang’anywa na wakulima mifugo yao zaidi ya ng’ombe 3,000 ambazo ziliswagwa na kupelekwa wilayani Igunga.
Nkhambaku alisema kutokana na tukio hilo, ilibidi kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya zote mbili Kishapu na Igunga walikaa kikao na kulijadili suala hilo kwa kulitafutia ufumbuzi, na kuwa waliwataka wafugaji na wakulima kuacha mapigano hayo ikiwa serikali inalitafutia ufumbuzi pamoja na kutenga maeneo ya kilimo na sehemu za machungo ya mifugo.
Baadhi ya wafugaji walisema mapigano hayo yalitokana na wakulima kulima mazao maeneo yote na kusababisha kukosa maeneo ya malisho, hivyo kuamua kutafuta haki yao kwa nguvu.
Mmoja wa wafugaji hao, Ndelanha Mahona, alisema ng’ombe zaidi ya 3,000 waliswagwa na kupelekwa Igunga, kitendo ambacho wafugaji hawakukubali na kusababisha mapigano hayo.
Wakulima walidai wafugaji hao wamekuwa wakipitisha mifugo yao katika mashamba na kulisha mazao yao, kitendo ambacho hawakukubaliana nacho kwa kuwasababishia hasara kila mwaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu, Justin Sheka, alisema mapigano hayo yamehatarisha amani kwa wananchi, huku akiwataja walionyang’anywa mifugo hiyo kuwa ni Ndelanha Mahona, Mbuta Madila, Silag’wan Hendeka, Gidi Babashi na Gilijisiji Gilawida ambaye alijeruhiwa kwa kuchomwa mkuki.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu, aliitaka serikali kulitafutia ufumbuzi suala hilo haraka kutokana na wananchi kuanza kuuana hovyo.
“Suala hili linahitaji ufumbuzi wa haraka, eneo hilo la Mbuga ya Magalata lilitengwa kwa ajiri ya machungio ya mifugo, lakini wakulima wamevamia eneo hilo wakidai na wao wana haki ya ardhi na kuanza kulima mazao, hivyo serikali haina budi kulitatua tatizo hilo haraka ili kuepusha mauaji,” alisema Ntelezu.
Kufuatia mapigano hayo, wakuu wa mikoa ya Tabora na Shinyanga wameunda timu ya watu 18 kuchunguza chanzo cha mgogoro huo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Nasoro Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa, walisema wameazimia kuwa wafugaji wa Kishapu wabaki katika eneo lao la Magalata wasivuke mto Manonga.
Walisema pia kwamba wakulima wa Igunga walioko katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa wabaki katika vijiji vyao na wasivuke mto Manonga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alisema msako unaendelea kuwabaini waliohusika na mapigano hayo.