KIPATO KIDOGO TATIZO KUJIUNGA MIFUKO YA JAMII.
From Mtwara By Hassan Simba.
IMEELEZWA kuwa kipato kidogo miongoni wa jamii ni moja kati ya sababu zinazochangia watu wengi kushindwa kujiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini na hivyo wengi wao kuishi katika maisha duni zaidi wanapokuwa wazee na kuishiwa nguvu ya kufanyakazi.
Hayo yameelezwa leo na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii SSRA. Irene Isaka, alipokuwa akitoa maelezo juu ya kazi za mamlaka hiyo kwenye mafunzo ya siku moja ya mamlaka yake kwa viongozi wa serikali, mashirika ya umma na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wa mkoa wa Mtwara, iliyofanyika katika ukumbi wa Boma mjini hapa.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa watu wengi wanashindwa kuchangia michango ya kila mwezi katika mifuko ya jamii licha ya serikali kuongeza wigo kwa wasio na ajira rasmi kujiunga na kunufaika na mifuko hiyo. Ambapo hata hivyo alisema ni jukumu la kila mfuko kuendelea kuwaelimisha ili waweze kuona umuhimu wa jambo hilo na kujiwekea kidogo wanachokipata kwa maisha yao ya baadae.
Isaka alisema kuwa hadi sasa wanachama wa mifuko ya jamii nchini wamefikia asilimia 1.8 kati ya nguvu kazi yote iliyopo nchini, ambapo michango ya wanachama ni shilingi trioni 1.6 huku mafao yaliyokwishakutolewa yakifikia trion 1.06.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hadi sasa mifuko ya jamii nchini inahudumia wastaafu 87,000 ambapo vitegauchumi vilivyowekezwa vinafikia thamani ya shilingi trion 4.9 na mali zilizopo zikiwa na thamani ya shilingi trion 6.4.
Akifungua mafunzo hayo mkuu wa wilaya ya mtwara, willman kapenjama Ndile alisema kuwa tabia ya baadhi ya waajili kushindwa kuwasilisha michango ya watumishi wao katika mifuko ya jamii kwa wakati ni dhuruma na inachangia kuwafanya wafanyakazi hao kuishi maisha mafupi mara baada ya kustaafu.
Ndile alisema kuwa iwapo waajili watakuwa makini na kuwasilisha michango kwa wakati mifuko hiyo itaweza kuwahudumia wanachama wake kwa wakati na hivyo kumuwezesha mstaafu kuendelea kuishi maisha mazuri na marefu kutokana na kuukimbia umasikini kwa kupata mafao yatakayomwezesha kujikimu.
Mwisho.
Jikiteni katika sekta binafsi;
Mtwara, By Hassan Simba.
MAMLAKA ya usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA), imeshauriwa kujikita zaidi kutoa elimu katika sekta binafsi kwani kwa kiwango kikubwa bado haijafikiwa na hifadhi ya mifuko ya kijamii pia ndiyo yenye watu wengi haswa vijijini.
Ushauri huo ulitolewa Lleo na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara . Wilman Ndile, wakati akifungua mafunzo ya siku mojaya hifadhi ya jamii kwa viongozi wa Mkoa wa Mtwara yaliyofanyika katika ukumbu wa Boma mjini hapa.
“Ningeshauri mjikite zaidi katika sekta binafsi ambapo vibarua pia wanaweza kuingia katika mifuko hii ya jamii kwani wapo wengi ambao wameajiriwa ajira za muda katika makampuni ya ujenzi hapo Mkoani kwetu…. Mfano wake hawa watu wa kiwanda cha saruji cha Dangote kina vibarua wengi wanaoweza kuwa wanachama wa mifuko ya jamii” alisema . Ndile na Kuongeza kuwa:
“Wenzetu nchi zilizoendelea wanajivunia kuwa na mifuko hii ya jamii ambapo kwao ina nguvu hivyo ujanja ni kuingia kwa wingi ili kuweza kunufaika katika mifuko hiyo ili kuendana na wakati wa sayansi na tekinolojia” alisema Mkuu huyo.
Aidha, katika kutoa mada kwa washiriki wa semina mkuu wa idara ya mahusiano ya jamii kwa umma na uhamasishaji wa mamlaka hiyo. Sarah Msika, alisema kuwa wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi wanatakiwa kuwa macho na maisha yao ya baadae kwani hayatabiriki hubadilika kila kukicha.
“Maisha yetu siku hizi hayatabiriki hivyo ni vizuri kujiunga katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa humo… kwani unaweza ukawa unapata fedha ya kutosha kama hutawekeza vizuri basi huwezi kujua kesho itakuwa vipi” alisema. Msika.
Hata hivyo aliowanyesha washiriki wa semina faida ya kuwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwani michango huwekezwa katika vitega uchumi mbalimbali kama majengo na akachukulia mfano wa Chuo Kikuu cha Dodoma kilijengwa na fedha za mifuko ya jamii na sasa kinanufaisha watu wengi kwa elimu inayotolewa chuoni hapo.
“Kuna faida kubwa kuingia katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii kwani fedha zake huwekezwa katika majengo na mabenki kama ilivyo Chuo Kikuu cha Dodoma kimejengwa kwa fedha hizo na sasa kinasaidia wananchi kupata elimu” alisema. Msika.