NI mkazi wa Rombo anayedaiwa kumtendea mkewe unyama huo kwa madai ya ulevi huku wengi wakilaani.
Rombo.Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mkazi mmoja wa Kijiji cha Kisare, Kata ya Kisare Msaranga wilayani Rombo mkoani hapa kwa tuhuma za kumfanyia mkewe kitendo cha kikatili kwa madai ya kumwingiza chupa ya soda sehemu za siri.
Tukio hilo linadaiwa kutendwa usiku wa Novemba 22, mwaka huu wakati wanandoa hao wakitokea harusini na ndipo inadaiwa kuwa mara baada ya kufika nyumbani mume huyo alimshika mkewe (Jina tunalihifadhi) kwa nguvu na kumshindilia chupa ya soda katika sehemu zake za siri na kumsababishia maumivu makali yaliyomsababishia majeraha.
Tukio hilo la kusikitisha lililothibitishwa na wakazi na majirani, pamoja na viongozi wa vijiji wa kata hiyo, limetokea wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia.
Wakizungumza na Mwananchi kijijini hapo jana, baadhi ya watu wakiwamo Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Kisare, Aloyce Mrosso, Ofisa Mtendaji Kata, Happymack Mrina na baadhi ya wanawake hawakupenda majina yao yatajwe kwa nyakati tofauti walisema, mtuhumiwa alikamatwa Novemba 23, akapelekwa Kituo kidogo cha Polisi cha Mashati wilayani humo.
Ofisa Mtendaji huyo alisema, tukio hilo la kinyama alilofanyiwa mwanandoa huyo mwenye watoto wanne wa kike mmoja na wa kiume watatu. Ukatili huo ni tukio lililokithiri kwenye kata hiyo na ni la kwanza la aina yake.
Mroso alisema, mama huyo alikwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Huruma wilayani humo ambapo inadaiwa alishonwa nyuzi kadhaa katika sehemu zake za siri.
Baadhi ya wanawake walionyesha hasira kali dhidi ya ukatili huo na walidai kuwa ni kawaida ya mwanaume huyo kumfanyia ukatili mkewe kwa kisingizio cha ulevi.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz hakuweza kuthibitisha hilo kutokana na kutopatikana kwa njia ya simu na hata ofisini kwake baada ya kupigiwa simu kwa muda mrefu licha ya kutumiwa ujumbe ambao hakujibu hadi taarifa hizi zikienda gazetini.
Hivi karibuni matukio mengi ya unyanyasaji pamoja na mauaji dhidi ya wanawake na watoto ya meiweka nchi njia panda.