STAA mkubwa wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza stone’ ambaye anasifika kwa ulevi wa kupindukia na hivi karibuni aliripotiwa kuacha, inadaiwa amerejea tena, safari hii kwa kiwango cha kutisha.
Chanzo makini kutoka ndani ya familia ya mwanamuziki huyo anayefanya kazi na bendi ya Extra Bongo, kimeliambia gazeti hili kwamba hali ya sasa ya Banza ni mbaya, kwani ulevi wake umemfanya kushindwa kabisa kufanya kazi.
“Banza amerudia tabia yake ya zamani, analewa sana mpaka anashindwa kufanya kazi jambo ambalo linaihuzunisha familia yake, afya yake imeanza kuzorota,”kilisema chanzo hicho.
Baada ya kuzinyaka habari hizi paparazi wetu alimtafuta Mkurugenzi wa Extra Bongo ambayo Banza anafanya nayo kazi, Ally Choki.
“Banza ni sikio la kufa, amerudia kunywa pombe yaani analewa sana, alianzia mikoani ambako tulienda kufanya shoo za pasaka hata kazi kwa sasa hawezi kufanya ndiyo maana hajaonekana jukwaani leo (Jumamosi iliyopita).
“Najiandaa kwenda kwa mama yake kumkabidhi ili ajue kwamba hayupo mikononi mwangu tena, asije kupata matatizo nikaulizwa mimi, Banza tumeshaongea naye sana kuhusu kuachana na pombe lakini hasikii wala haelekei sasa mimi sina la kufanya zaidi ya kwenda kumkabidhi kwa mama yake,”alisema.
Juhudi za kumpata Banza ili kuzungumzia tuhuma hizi ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani.
-GPL