FILAMU mpya iliyochezwa na aliyekuwa mwongozaji na mwigizaji wa sinema za Bongo, Adam Kuambiana, iitwayo ‘Stupid Father’ ipo mbioni kukamilika na kuingizwa sokoni mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mhariri wa filamu hiyo, Danis Ngakongwa, alisema kuwa wanatambua sinema hiyo inasuburiwa kwa shauku kubwa na wadau nchini kwa lengo la kuangalia namna Kuambiana alivyocheza, kwani amefariki akiwa katika kiwango cha juu cha uigizaji.
Nipo katika hatua za mwisho za kukamilisha kuihariri filamu ya ‘Stupid Father’ ili tuiweke sokoni, kwa sababu wadau wamekuwa wakiiulizia kwa lengo la kutaka kuona jinsi alivyocheza, kwani wakati anaanza kuonyesha ustadi wake wa kuigiza mauti yakamchukua,” alisema Ngakongwa.
Katika hatua nyingine, Ngakongwa alitoa salamu za rambirambi kwa kifo cha mkongwe wa maigizo ya vichekesho, Said Ngamba, maarufu kwa jina la Mzee Small, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Ngakongwa alisema kuwa tasnia ya filamu imeanza kupata pigo kutokana na kuondokewa na waigizaji wake waliokuwa wanategemewa katika fani hiyo na hawana cha kufanya kutokana na jambo hilo kuwa nje na uwezo wao.