` |
Mwili wa Daniel Anael Lema, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya sheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mt. Augustino, Tawi la Iringa (Ruaha University College - RUCO) umeagwa leo na kusafirishwa kuelekea mkoani kwao kilimanjaro kwa mazishi.
Wanafunzi kadhaa wa chuo hicho na baadhi ya wananchi wa manispaa ya Iringa waliogusa na tukio hilo walijitokeza katika hospitali ya mkoa wa Iringa ambako shughuli ya kuuga mwili huo ilifanyika.
Jeshi la Polisi mkoani iringa linawashikilia watu wanne ambao ni walinzi wa Juka usalama waliokuwa wakilinda nyumba moja ya kulala wageni iliyopo kihesa katika manispaa ya iringa kwa madai ya kumchoma moto mwanafunzi huyo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa Ramadhani Mungi alisema tukio hilo lilitokea Juni 24 majira ya saa tisa usiku baada ya wasamaria wema kutoa taarifa polisi kuwa kuna mtu anatembea akiwa anawaka moto.
Mungi alisema mara baada ya kupata taarifa hiyo Jeshi la Polisi lilifika katika eneo hilo na kumkuta Daniel Lema (25) akiwa ameanguka chini huku akiwa amefungwa mikono nyuma.
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa hao waliomchoma moto kuwa ni Mussa Nganga (28), Costa Mgayuka (38), Steven Kalole (24) na Samson Peter (24) wote wakazi wa Kihesa waliokamatwa kabla ya kutoweka mjini iringa .
“Tulipopata taarifa tulifika eneo hilo kwa haraka na tukamkuta ameanguka chini tulimfungua ile mikono na kumchukuza vizuri tulimkuta akipumua kwa shida ndipo tukamkimbiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya kupata matibabu.”alisema Kamanda Mungi
Alisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa baa moja inayoitwa In box bar inayomilikiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Frederick Mwakalebela akipata kinywaji huku angiangalia michuano ya mpira wa miguu (kombe la dunia) ambayo inaendelea nchini brazili.
“Mwanafunzi alikuwa anaangalia michuano hiyo ya mpira wa miguu kwenye baa hiyo na baada ya mpira huo kuisha aliondoka na kuelekea nyumbani kwako Kihesa kabla ya kufika nyumbani eneo hilo kuna nyumba ya kulala wageni iitwayo Glory lodge ambapo pembeni yake kuna grocery moja iitwayo Glory grocery akaingia hapo akifikiri ipo wazi ili aendeleze kinywaji,” alisema.
Alisema wakati akigonga mlinzi wa nyumba ya kulala wageni Glory lodge ambae ni mmasai aitwaye Mussa Nganga alimuona na kumuita ndipo kijana akakimbia na baada ya kukimbia alimfukuza na kuwaita wenzake watatu na kumfanyia kitendo kama hicho.”alisema Mungi .
Baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa, Lema aliendelea na matibabu yake mpaka alipokutwa na mauti jana majira ya saa nane mchana.