Quantcast
Channel: Blogu ya Wananchi
Viewing all articles
Browse latest Browse all 32622

EXCLUSIVE PART 3 YA NINI KILIMUUA MWANAMUZIKI MAARUFU WA VIJANA JAZZ CHIRIKU HEMEDI MANETI? LIVE FROM HIS BEBZ!!

$
0
0




Imeandikwa na MOHAMMED KUYUNGA
KIDA Waziri  (pichani juu)anasema kabla ya kupelekwa Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupimwa, alifanya jitihada za kwenda Hospitali ya Mwananyamala  kwa lengo la kumtafuta daktari aliyemtibia marehemu Maneti.
Jitihada zake hizo zilifanikiwa na akaweza kumpata, lengo lake lilikuwa ni kumuuliza kuhusu kile kilichomuua Maneti ili awe na uhakika hata kabla ya kwenda kupimwa.
“Nilimuuliza ili aniambie Maneti amekufa kwa ugonjwa gani lakini alishindwa kuniambia chochote zaidi ya kuniuliza kama miye ndiye Kida Waziri zaidi ya hapo hakuonesha ushirikiano. Basi hakuendelea kuniambia zaidi kwa hiyo naweza kusema kuwa jitihada zangu hazikuweza kuzaa matunda.
“Sikuona kwa nini nisumbuke, nikaamua kuachana na daktari yule na kuendelea na maisha yangu,” anasema.
Ashushwa jukwaani
Siku moja aliamua kupitia katika bendi yake ya Vijana Jazz kwa lengo la kusalimiana na wanamuziki wenzake.
Vijana walikuwa wakifanya onyesho lao katika Ukumbi wa Vijana Social Club Kinondoni , akiwa ukumbini humo baadhi ya wapenzi wakamuomba apande jukwaani ili aweze kuimba baadhi ya nyimbo zake ambazo zilipata umaarufu lakini  Kida akiwa jukwaaani akijiandaa kuimba, muziki ulizimwa.
“Mashabiki wengine wakanitolea maneno makali sana kwa kuniambia kuwa miye siyo mwanamuziki, najua walikuwa wamekasirika kwa kufahamu kwamba nimehamia Roots & Culture,” anasema Kida Waziri.
Viongozi wamwita pembeni
“Viongozi wa bendi wa wakati huo, Rashid Pembe na John Kitime walikuwa watu wazuri sana, waliniambia kuwa baadhi ya viongozi wa utawala hawataki nipande jukwaani, sikujua sababu na viongozi hao wala hawakuniambia, basi nikashuka na kuendelea na mambo yangu mengine,” anasema.
Mwanasiasa atoa shinikizo
Mwanasiasa ambaye kwa sasa ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( jina lake bado tunalihifadhi), alimshinikiza Kida kwenda katika Hopsitali ya Hindu Mandali ili kuweza kumwona daktari anayeweza kumpa majibu ya ugonjwa wake.
“Alinitajia jina (tunalo na tunalihifadhi) na hata nilipofika katika hospitali hiyo nilikutana na daktari huyo ambaye alionekana kuwa na taarifa zangu za kufika hospitalini hapo mapema kwa kuambiwa na mwanasiasa.
“Daktari aliniambia kuwa alikuwa na taarifa na kile kilichomuua Maneti kutoka Hopsitali ya Mwananyamala na taarifa ni kwamba, Maneti alifariki dunia  kwa Ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Kida ambaye alifadhaika alipoambiwa maneno hayo.
Akutwa na virusi vya Ukimwi
Daktari huyo alimpa majibu Kida na kwambia kuwa ameathirika na ugonjwa wa  huo ambao hauna kinga wala tiba.
“Daktari alinipa majibu akaniambia kuwa nimeathirika na kuniambia kwamba nisikate tamaa kwa kuwa hata yeye aliwahi kuwa na mtu ambaye ameathirika lakini kwa bahati nzuri yeye amepona.
 “Hakunipa ushauri wowote, zaidi ya kuniaambia kwamba amegundua kuwa nimeathirika na kuniambia kuwa hata mwanangu naye atakuwa ameathirika.
“Nilisikia ganzi mwilini mwangu kwa muda, lakini kwa kuwa nilishashambuliwa vya kutosha sikuweza kuumia sana tayari imani ya moyo ilishavunjika na nilijiona mdogo kama sisimizi na kukosa nguvu.
“ Niliyakumbuka maneno  aliyoaniambia Maneti  siku ile kwamba, kama kufa yeye hatakufa kwa Ukimwi bali ni kwa ajili ya watu na jinsi alivyokuwa akilalamika na kunitaka kuwa makini na watu... nilijiuliza  maswali  mengi sana nikakosa majibu,” anasema.
 “Nilirudi nyumbani na kuwaambia baadhi ya ndugu zangu kile nilichoambiwa na daktari kwamba nimeathirika na ugonjwa huo ambao hauna tiba.
“Ndugu zangu walinilaumu kwa uamuzi niliouchukua wa kwenda peke yangu hospitali.Wengi walifadhaika na kuna wakati walikuwa wakijificha pembeni na kuanza kulia, nilipowaona na kuwauliza walichokuwa wakilia, hawakuniambia ukweli, walinidanganya kwamba kulikuwa na taarifa za msiba lakini nilijua kuwa walikuwa wamefahadhaishwa na kile  nilichowaambia kwamba  nimeathirika,” anasema.
Kida anasema kuwa ndugu zake hao walikuwa wakiumia kwa kuwa walikuwa wakipata misukosuko kutoka kwa watu mbalimbali mitaani.
“Kuna wakati mwingine walikuwa wakitaka kupigana kwa sababu yangu kutokana na maneno ya watu waliokuwa wakinizungumzia vibaya ingawaje wao hawakuwa wakiambiwa maneno makali kama yale niliyokuwa nikiambiwa miye,” anasema.
Mbunge ampeleka kwa mganga
Mwanasiasa aliyekuwa mstari wa mbele kufuatilia suala hilo, (mbunge) akamtaka Kida kwenda kupata tiba Kariakoo kwa Mwanamke aliyekuwa maarufu kwa tiba za asili kipindi hicho, Bi. Hawa Nyamichwo ambaye alikuwa akipatikana Kariakoo jijini Dar es Salaam.
“Aliniambia kuwa ninaweza kupona kwa kuwa Bi. Hawa Nyamichwo amewasaidia wengi kuweza kupona ugonjwa huo, kikubwa ambacho nilikuwa naaminishwa ni kwamba Maneti alichelewa kutibiwa  kwa kuwa nimewahi, basi ninaweza kupona.
“Hata ndugu zangu waliafika kwenda kwa mganga huyo wa tiba za asili na kuweza kupata tiba kwa kuwa nao walikuwa wamesikia sifa zake kutokwa kwa watu mbalimbali,” anasimulia Kida.
“Mpaka hapo, mipango ya safari ya kwenda Austria ilikuwa imeonekana kama vile imefikia ukingoni, kwa sababu kipindi kile ukiwa na ugonjwa huo ilikuwa ni vigumu kusafiri kwenda nje .
Atarudi maiti
Katika kushindilia msumari katika kidonda, baadhi ya watu walisema kuwa kama Kida atasafiri na Roots & Culture kwenda Austria basi atarudi  maiti na kuwapa gharama ya kuurudkisha mwili wake Tanzania.
“Maneno mengi yalikuwa ni ya kukatisha tamaa ili nisiende safari hiyo  lakini namshukuru sana Jah Kimbute hakutaka kusikiliza maneno ya watu wengine, “ anasema
Apelekwa kwa mganga
Kida anasema kuwa kwa kuwa hakuwa na  fedha mbunge alimpeleka kwa  mganga wa tiba za asili Bi. Hawa Nyamichwo na kisha akapewa  dawa za majimaji zilizowekwa katika chupa za plastiki na kutakiwa kunywa mara nne kwa siku.
Dawa nyingine zilikuwa ni za mwanaye Cecilia ambaye alitakiwa kupakwa na kunyweshwa ili kuwa kama kinga na tiba yake ya ugonjwa huo wa ukimwi.
Ndoto ya ajabu
Kida anasema maisha yake yalikuwa yametawaliwa na wasiwasi mwingi na kuna wakati alikuwa akiogopa hata kukaa au kulala  peke yake chumbani kwake.
“Nilikuwa nahisi kama kuna mtu alikuwa akichungulia chumbani au  kunifuatilia nyendo zangu,  mpaka leo hii sijui kwa nini nilikuwa hivyo. Usiku mmoja niliota ndoto ambayo mpaka leo hii siijui maana yake ni nini, nilimuota  Mbunge huyo aliyekuwa akipinga nisisafiri kwenda Austria akiwa sehema na kuwauliza watu ulipo mwili wa Maneti.
“Nilimuota akimtaka mtu amwonyeshe mwili wa Maneti, kisha akamwambia mtu huyo kwamba ahakikishe anaulinda mwili huo ambao ulionekana kuwa mdogo na kuingizwa katika jeneza lenye ukubwa wa kibiriti.”
Waziri akoa jahazi
Baada ya taarifa hizo mmoja wa mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (mpaka leo hii bado ni waziri, jina lake tunalihifadhi pia) aliingilia kati suala hilo na kusema kuwa lazima Kida asafiri  kwenda Austria.
“Waziri huyo alikanusha madai ya Maneti kufa kwa Ukimwi na kusema kuwa wala haukuwepo mpango wa kumchukulia dawa za Kemroni kutoka Kenya wakati alipokuwa akiumwa.
Nini kiliendelea?  Usikose sehemu ya nne ya  simulizi hii  ya ukweli ya yaliyomkuta mwanamuziki Kida Waziri.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 32622

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>