MTOTO mwenye umri unaokadiriwa kuwa mwaka mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, aliokotwa huko Kibamba CCM, jijini Dar es Salaam, nje ya geti la nyumba ya Getruda Gervans.
Tukio hilo lilitokea Juni 24, mwaka huu saa moja na nusu asubuhi huku mfuko wenye nguo zake ukiwa pembeni yake.
Kwa mujibu wa mama mwenye nyumba hiyo, baada ya kumuokota, alimpeleka Kituo cha Polisi Mbezi ambako nako walimpeleka katika Hospitali ya Mwananyamala kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.
Afisa ustawi wa Jamii wodi ya watoto Muhimbili, Grace Julius alilithibitishia gazeti hili kumpokea mtoto huyo Juni 25, mwaka huu akitokea Hospitali ya Mwananyamala na akatumia fursa hiyo kulaani tabia ya kutupa watoto.
Aidha, aliomba mtu yeyote mwenye taarifa ya kupotea kwa mtoto sehemu yoyote kufika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alisema kwa taarifa zaidi apige simu namba 0788366399.
Mhariri: Tunakemea vikali vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto na tunawaomba wananchi kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka zinazohusika endapo watamuona mtu yeyote akiwanyanyasa au kuwafanyia ukatili wowote watoto.