Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic ameanza kazi kukinoa kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara katika uwanja wa Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
KOCHA wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic ameanza kazi kukinoa kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara katika uwanja wa Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Loga ameamua kuanza kambi mapema kwa lengo la kurejesha heshima ya Simba iliyopotoea kwa miaka mitatu mfululizo.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa zamani ambao hawapo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya Julai 20 dhidi ya Msumbiji wanahudhuria pamoja na wachezaji wapya.
Mshambiliaji wa zamani wa Supersport United ya Afrika kusini, Dani van Wyk amekuwa akihudhuria mazoezi hayo kama sehemu ya kujaribiwa na Loga kabla ya kufanya maamuzi ya kumsaininisha mkataba.
Mchezaji huyo amekuwa akijitahidi kuonesha uwezo wake, lakini Loga anasema anahitaji muda kumtazama kabla ya kufikia makubaliano.
Mlinda mlango bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita, Hussein Sharrif `Iker Casillas` amesharipoti kuanza mazoezi na Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar.
Wachezaji wengine wapya walioanza mazoezi ni pamoja na Michael Mgimwa kutoka Thailand, Mohammed Hussein maarufu kama Tshabalala kutoka kwa `wanankulukumbi`, Kagera Sugar.
Wakati Simba wakiendelea na mazoezi hayo, nao watani wao wa jadi, Yanga sc wanaendelea kunoa makali katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola chini ya kocha mkuu, Mbrazil Marcio Maximo akisaidiwa na Leonardo Neiva.
Katika harakati zake za kufanya vizuri msimu ujao, Yanga imewanasa nyota wawili kutoka Brazil, kiungo mshambuliaji, Andrey Coutinho aliyewasili siku moja baada ya Maximo kutua nchini kutokea nchini Brazi.
Mshambuliaji mwingine kutoka Brazil, Geilson Santos Santana `Jaja` aliwasili jana akitokea mjini Sao Paul nchini Brazil tayari kwa kuanza kazi Dar Young Africans.
Jaja alikuwa anacheza timu ya Itabaina FC ya nchini Brazil na ujio wake unafikisha idadi ya Wabrazil wanne katika kikosi cha Yanga , (makocha wawili na wachezaji wawili).
Asubuhi ya leo, Jaja anatarajia kuonekana kwenye mazoezi ya Yanga katika shule ya sekondari Loyola.
Usajili wa Yanga umevuta hisia za mashabiki wengi na kupandwa na `midadi` ya kukiona kikosi hicho msimu ujao wa ligi kuu unaotarajia kuanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu.
Yanga ya Maximo inatarajiwa kubadilika kimfumo na nidhamu ya wachezaji kwa ujumla. Maximo ni kocha mwenye msimamo mkali, anapenda nidhamu ya wachezaji uwanjani na nje ya uwanja. Hapendi kuingiliwa katika maamuzi yake.
Hii ilionekana alipokuwa na timu ya Taifa ya Tanzania kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010. Mara nyingi Maximo aliweka wazi kuwa kama mchezaji hana nidhamu, hawezi kucheza katika kikosi chake. Kwa muda mrefu walitofautiana na aliyekuwa kipa namba moja wa Tanzania, `Tanzania One`, Juma Kaseja kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Hata wakati Mrisho Ngassa anaitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Taifa stars na Maximo, kocha huyo alionesha msimamo wake licha ya watu wengi kushinikiza winga huyo ajumuishwe kikosini.
Maximo aliweka wazi kuwa anahitaji kumuona Ngassa kwenye mechi zaidi ya moja ili ajiridhishe. Mashabiki walipiga kelele kwasababu Ngassa alikuwa kwenye kiwango cha juu, lakini alimuita mpaka alipojiridhisha.
Haruna Moshi `Boban`, Athuman Idd `Chuji` waliwahi kukumbana na joto la jiwe kutoka kwa Maximo kutokana na utovu wa nidhamu.
Ipo mifano mingi ya kutolea kuhusu Maximo, lengo likiwa ni kuonesha jinsi anavyoamini katika nidhamu ya wachezaji.
Huyu ni kocha anayeiamini falsafa yake. Wachezaji wa Yanga watalazimika kuwa wapole kwa Mbrazil huyu. Longo longo za utovu wa nidhamu si rahisi kusikika kwa Maximo.
Wakati Maximo akisifika kwa kuzingatia nidhani, kwa mwenzake Logarusic wa Simba hali ni kali zaidi.
Loga ni moto wa kuotea mbali. Tangu ajiunge na Simba mzunguko wa pili wa msimu uliopita akirithi mikoba ya Abdallah Kibadeni, Mcroatia huyo aliwawashia indiketa nyekundu wale wote waliopuuza maelekezo yake.
Loga haoni shida kumchomoa mchezaji uwanjani ndani ya dakika tatu. Huwa hana subira pale mchezaji anapovurunda. Betram Mwombeki, Henry Joseph Shindika, na wengineo wanalijua vizuri hilo.
Loga alifika mbali zaidi kwa kuweka masharti magumu kwa wachezaji akiwemo kukatwa mishahara na posho wanaposhuka viwango, kufika mazoezini nusu saa kabla ya muda wa mazoezi na mchezaji akifika uwanjani, lazima uwe unachezea mpira kuweka mwili sawa na si kukaa na kupiga domo tu.
Wachezaji waliona Loga hafai na mara kadhaa waliibua maneno ya chinichini wakisema kocha huyo ni mkali mno.
Hata hivyo, uongozi wa Simba uliwapuuza na kumuonezea mkataba wa miaka miwili zaidi. Loga ni muumini wa nidhamu kwa kiasi kikubwa na ana msimamo mkali.
Marcio Maximo na Dravko Logarusic wanafanana kwa kuzingatia nidhamu na kusimamia misimamo yao. Ni makocha wanaopenda kutekeleza falsafa zao bila kuingiliwa.
Kwa aina hii ya makocha, Simba na Yanga zinaweza kufanana kwa nidhamu, lakini viwango vya uchezaji vinaweza kuwa tofauti kutokana na aina ya wachezaji walionao.
Simba ya Loga, Yanga ya Maximo, kuna kitu kipya kitaonekana kuanzia septemba 20, mwaka huu. Acha tusubiri kuona mbwembwe za watani wa jadi.