Quantcast
Channel: Blogu ya Wananchi
Viewing all articles
Browse latest Browse all 32622

LE MUTUZ LIVE MY ARTICLE ON JAMBO LEO NEWS PAPER OF 22/12/2013

$
0
0



PICHA KUBWA NI KAMA MWIGULU ANA HOJA  NA SI VINGINEVYO!.


Wiki kama mbili zilizopita Wa-Tanzania tuliamshwa na maneno makubwa na mazito sana kwenye kichwa cha habari za gazeti moja maarufu sana hapa nchini likiwa na habari za Waziri mmoja wa zamani ambaye bado ni Mbunge, likimtuhumu sana kuhusika na msichana mdogo huku akiwa na mke. Magazeti mengine karibu yote hayakuonyesha nia ya kuibeba habari hiyo ambayo gazeti hilo liliendelea kuibeba siku moja baada ya nyingine, hatimaye gazeti moja la udaku nalo likajiunga katika wimbo huo na hata kwenda mbali kidogo na kuanza hata kukishambulia chama cha Mbunge huyo likikiunganisha kuhusika na tuhuma hizo. Hatimaye gazeti la udaku likagundua ukweli tofauti na ukweli wa mwanzoni wa habari hiyo na kuuweka wazi kwenye kurasa zake za mwanzoni sana, lakini gazeti hilo lingine likaendelea na kupiga sana makelele huku likidai kwamba hata kama hakuna kesi kwa Mbunge huyo lakini kutuhumiwa kwake na vitendo hivyo na huku ana mke na watoto kwa kiongozi kama yeye ilikuwa ni dhambi kubwa sana kisiasa.

  Majuzi tena wananchi wa Taifa hili tumeshuhudia malumbano mengi ndani ya bunge baina ya Wabunge wa CCM na Upinzani hasa wa Chadema, wakilumbana sana bungeni kwa hoja nyingi ambazo baadhi ya wananchi katika jamii yetu nao pia wamekuwa katika malumbano makubwa sana kuhusu uhalali wa baadhi ya hoja ambazo wabunge hao wamekuwa wakipigania huko bungeni Dodoma. Na hoja iliyoleta kizaa zaa sana ni ile ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM na Mbunge wa chama hicho aliyeomba muongozo wa Spika  kuhusu uhalali wa kitendo cha Kiongozi wa upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, kumkatiza kufanya kazi za wananchi mbunge wa Viti maalum wa chake aliyekuwa New York City, Marekani kikazi na akiwa amelipwa posho kamili kwa ajili ya safari hiyo ya kikazi na kumtaka arudi Dubai mara moja ambako angekutana na Mwenyekiti huyo wa chama chake ambaye kwa maneno ya Mheshimiwa huyo, ni kimada wa muda mrefu wa Kiongozi huyo wa upinzani mpaka kufikia kuwa na mtoto naye huku inafahamika wazi kwamba ameoa na ana watoto. Hoja hii ilileta kizaa zaaa kikubwa Bungeni na hata nje ya bunge kutokana na baadhi ya wananchi kudai kwamba yalikuwa ni mambo ya binafsi na huku wengine wakidai ni hoja ya msingi sana kwa maadili ya uongozi wa Taifa na kuna hata walioenda mbali na kudai kwamba kuna Viongozi wa CCM ambao pia wana matatizo kama wanavyomtuhumu nayo Mwenyekiti wa Chadema.

Si kawaida yangu kuchambua au kujadili mambo ya binafsi ya wananchi au viongozi wao na hasa yanapokuwa hayahusiani na majawabu kwa maendeleo ya taifa lao, lakini ishu inapotokea katika muhimili muhimu kama wa Bunge la Jamhuri yetu huku likiwagusa viongozi wetu maarufu na watunga sheria zetu zinazotumika sasa na kwa vizazi vijavyo, kama mwananchi wa taifa hili mwenye upeo mkubwa kuona mbali inanilazimisha kuijadili na kuichambua kwa kina hoja hii ya viongozi wetu na kutokuwa waaminifu kwa familia zao na maana yake kwa uongozi wao kwa taifa letu. Hoja hii imeibuliwa wakati wa mjadala mzito sana wa matumizi mabovu ya baadhi ya wabunge kwa pesa za walipa kodi kwa kuchukua posho za safari ambazo wengi wao hawaendi au hawakai kwa muda waliouchukulia pesa hizo. Na cha kustaajabisha kuliko ni pale gazeti lile maarufu lililomtuhumu sana Mbunge wa CCM siku chache za nyuma kuhusu hoja kama hii, lilipoamua kutoigusa kabisa habari hii mpya inayomgusa Kiongozi wa Upinzani bungeni ambaye ndiye mmiliki wa jengo lenye ofisi za Makao makuu ya gazeti hilo la kila siku.

Tabia ya viongozi wa juu wa wananchi kukosa uaminifu kwa familia zao ina historia ndefu sana sio hapa tu bali hata nje ya taifa letu, lakini imekuwa ikichukuliwa kwa mtizamo tofauti kwa mfano Wa-Faransa ni taifa moja ambalo limejitenga na mataifa mengine makubwa ya magharibi katika ishu hii kwa kuikumbatia kuwa ni ya kawaida sana lakini sio kwa mataifa mengine ya huko kama Uingereza na Marekani. Mwaka 1966 wakati Rais mashuhuri wa Ufaransa alipokuwa anazikwa Mke wake Danielle alishirikiana sana na hawara wa muda mrefu sana wa Mumewe Anne Pingeot ambaye pia alikuwa amezaa naye mtoto wa kike mkubwa Mezzarine. Taifa zima la Ufaransa lilikuwa linajua wazi kwamba Rais huyo alikuwa na familia mbili moja ya mke wake wa ndoa na nyingine ya haramu, lakini bado Rais huyo aliweza kuchaguliwa kuongoza Taifa hilo na kupewa heshima za pekee sana siku alipokuwa anazikwa. Na hata baada ya Rais huyo kutoka waliomfuatia wote kina Jacques Chirac na Sakozy walikuwa sio waaminifu kwa familia zao na taifa hilo halikujali, kwa mfano baada ya kumaliza muda wake wa Urais aliandika kitabu cha kumbu kumbu yake akisema kwa kujigamba sana kwamba "Kuna wanawake niliowapenda sana nikiwa Rais na wala haikuwa siri kwa wananchi" haya ni maneno ambayo kwa nchi kama Marekani na Uingereza ungekua ndio mwisho wa kufanya siasa. Wafaransa mpaka leo hawaelewi ni kwa nini raia mwenzao aliyekuwa Rais wa Shirika la Fedha la dunia IMF Kraus Khan, alipatwa na matatizo makubwa sana nchini Marekani kuhusiianan na kesi ambayo haikutihitishwa ukweli wake kwamba alimbaka msichana mmoja akiwa mjini New York City, USA na kuishia kuachishwa uongozi huo na hata kumuwia vigumu kugombea Urais wa Taifa hilo nafasi ambayo alikuwa akitabiriwa sana na taifa lake kushika nafasi hiyo baada ya Rais Sarkozy. Wafaransa wanaamini kwamba ni muhimu sana kwa mwanaume kutokuwa muaminifu kwa ndoa yake ili kuilinda ndoa hiyo idumu kwa muda mrefu kuepuka matatizo ya ndoa hiyo.

Lakini kwa Wamarekani na Waingereza wao wana mtizamo tofauti kabisa kuhusu suala hili la kukosa uaminifu kwa viongozi wao kwa familia zao, wakiamini kwamba kunaweza kuathiri sana uwezo wa kiongozi huyo kusimamia haki na ukweli kwa taifa lake na kwamba sio rahisi kwa kiongozi asiyekuwa muaminifu kwa familia yake kuweza kuwa muaminifu kwa wananchi na taifa lake. Kwa mfano Rais wao Bill Clinton mwaka 1998 alikuwa ni kiongozi wa kwanza wa taifa hilo kuhukumiwa kuondolewa madaraka na bunge la chini la taifa hilo Congress, lakini akaishia kupona kwenye bunge kubwa la nchi hiyo yaani Senate. Kaka Rais wa zamani wa Taifa hilo Bob Kennedy akiwa anaongoza kwa kura za maoni nchini kuwa Rais mnamo mwaka 1970 ghafla akakutwa na kshfa kama hii ya kukosa uaminifu kwa familia yake aliishia kujitoa kabisa kwenye mbio hizo za urais wa taifa hilo kubwa na lenye nguvu kuliko yote duniani. Na Uingereza nao ni kama ilivyo kwa taifa hilo kongwe wao pia viongozi wao wengi sana wamelazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kukutwa na kashfa za kukosa uaminifu kwa familia zao, jamii ikiongozwa na media za nchi hizo zikidai kukosa kwao maadili ya kuwa na nguvu kama kiongozi kwa jamii zao baada ya kukutwa na hizo kashfa. Hapa nyumbani mpaka leo bado tunahangaika na dhana hii, ambayo hivi karibuni imepata sura mpya ya kutegemea nani anaibebea bango na kwa masilahi ya siasa za chama gani.

Kwa mara ya kwanza kashfa kama hii kuzungumziwa katika siasa za Taifa ilikuwa ni mwaka 1995, alianza Baba wa Taifa kwenye mkutano wake maarufu na waandishi wa habari Kilimanjaro Hotel alipozungumzia hatma ya uongozi wa Taiafa hili na kutuhumu baadhi viongozi wa awamu ya pili kwamba baadhi yao hawakuwa waaminifu kwa familia zao sasa iweje wawe waaminifu na taifa. Uzito wa Baba wa Taifa kisiasa ulichangia kwa sehemu kubwa hoja na kuwapelekea kuondolewa uongozi kwa baadhi ya Viongozi hao waliotuhumiwa na Mwalimu, lakini kwenye uchaguzi wa Rais hoja hii ilipojitokeza tena kwa mmoja wa wagombea wa Urais wa Upinzani aliyesadikiwa kuwa na nguvu kubwa ya kukubalika na wananchi kwa wakati ule kwamba alikuwa na kimada nje ya mke wake wa ndoa. Hata hivyo hoja hiyo haikushika sana nguvu kwa wananchi wapiga kura kama vile hoja hiyo ilipokuwa imeshikiliwa na Baba wa Taifa dhidi ya Viongozi wa awamu ya pili na hivyo kihistoria kuifanya hoja hii kuwa na tabia ya kujali nani anaibeba katika ulingo wa siasa za taifa letu. Kurudi tena kwa hoja hii majuzi ni dalili za kwamba bado hii hoja ipo na kuna siku itakuja kuwa na nguvu kama kipimam joto cha wananchi kuhusu uaminifu wa Kiongozi wanayemtaka kuongoza Taifa. Majibu mazito sana ya Wabunge wa pande zote mbili kulaaani hoja hii kwamba haina mashiko wala tija kwa Taifa na wananchi wake ni dalili tosha kwamba Tanzania bado hatujawa tayari kuitumia hoja hii kama wenzetu wa Marekani na Uingereza. Wa-Tanzania bado hatujaona uhusiano wa aina yoyote kati ya tabia za kukosa uaminifu kwa familia kwa Kiongozi wetu wa Taifa kuwa na uhusiano wa aina yoyote na uaminifu wa Kiongozi huyo kwa wananchi na masilahi ya Taifa na hivyo kutufanya Wa-Tanzania katika mstari mmoja na wafaransa. Kuna mifano mingi sana ya kitafiti wa kisayansi unao onyesha kwamba Viongozi wasio waaminifu huwa wanaishia kutokuwa waaminifu kwa wananchi waliowachagua na Taifa lao, na pia kuna matokeo mengi ya utafiti wa kisayansi pia unaoonyesha kwamba sio hoja nzito sana Kiongozi anaweza kukosa uaminifu kwa familia yake na bado akawa kiongozi bora sana kwa taifa kama alivyokuwa Rais Bill clinton wa Marekani anayekubalika na wasomi karibu wote wa historia ya nchi hiyo kuwa ndiye Rais bora kuliko marais wote waliowahi kuongoza Taifa hilo lenye umri wa miaka takribani 300 sasa kwani ndiye Rais wa kwanza kuweza kuondoa deni la Taifa katika historia ya marais wote 44 waliowahi kuongoza nchi hiyo.

Kwa kumaliza naomba kusema kwamba kwa sasa hii hoja inaendelea kuwa ni tatizo la binafsi la kiongozi, familia yake na hasa Mungu wake, kama taifa bado hatujaikubali kuwa ni moja ya vigezo vya uongozi wa juu wa taifa letu, wananchi wengi wa Tanzania hawataki hata kuijadili wakidai kwamba ni mtego wa panya ambao unaweza ukasomba wote waliomo na wasiokuwemo kwa sababu nani atamfunga paka kengele kwa maana ya kwamba karibia wote ni wapungufu sana na hasa kwenye hoja hii. Baraza la Seneti la Marekani lilithibitisha ukweli huu baada ya kumuachia Bill Clinton amalizie muda wake wa urais  hata baada ya kuhukumiwa kuondolewa na Congress ya taifa hilo mwaka 1998. Baraza hili lilisema kwa kauli moja ya wajumbe wake 100 kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuoanisha makosa ya kukosa uaminifu kwa familia yake kwa Rais, kulikuwa na uhusiano wa aina yoyote na uwezo wake wa kuongoza Taifa hilo lenye nguvu kuliko mataifa yote duniani na kwamba wajumbe hao walikuwa wanahitimisha tu maoni ya wapiga kura wengi wa majimbo yao ya uchaguzi waliotaka wajumbe hao kumuachia Rais huyo mara moja. Na moja ya sababu kubwa iliyotolewa na wananchi wale wa Taifa lile kubwa ni zile zile zinazotolewa na wananchi wengi wa Taifa hili changa kwamba wote tukichunguzwa hakuna wa kupona kuhusiana na hoja hiyo ya kukosa uamnifu kwa familia na ndoa zetu. Kwa hiyo kwa sasa mpaka tutakapokuwa tayari kuikabili hoja hii bado ni hoja ya binafsi, ingawa inaweza kuwa na nguvu katika siasa zetu kwa kutegemea nafasi ya anayeibeba katika siasa zetu hapa nchini, gazeti la Tanzania Daima lilipojaribu kuibeba hoja hii halikuweza kushawishi jamii yetu kwamba kuna tatizo ni mpaka majuzi ilipobebwa na Kiongozi wa juu sana wa chama tawala bungeni ndipo ikawa  na nguvu na hata kumpelekea muhusika kutosikika kabisa kwa muda sasa ikiwa ni dalili tosha kwamba imempunguza nguvu za kisiasa kwa sasa. Lakini ni muhimu sana kwa viongozi wa Taifa letu wakajipima wenyewe na kuamua kama hoja hii iwe na mashiko katika uongozi wao wa kila siku kwa wananchi na Taifa letu, je kama huwezi kuwa muaminifu kwa familia yako mwenyewe utaweza kuwa muaminifu kwa wananchi waliokuchagua na hasa masilahi ya Taifa lao?


MUNGU IBARIKI TANZANIA

William John Samwel Malecela + 255 717 618 997
willymalecela.blogspot.com au willymalec@gmail.com


Viewing all articles
Browse latest Browse all 32622

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>