KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekutana wikiendi iliyopita na kufikia uamuzi wa kuwapa ajira aliyekuwa katibu wa Yanga, Selestine Mwesigwa na wa Simba, Evodius Mtawala.
Mwesigwa atafanya kazi hiyo chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi sita na endapo TFF atamudu nafasi hiyo atapewa muda zaidi, lakini kama atashindwa basi ajira yake itasitishwa mara moja.
Wakati Mwesigwa akiinasa ajira hiyo aliyoshindania vikali na Michael Wambura, mwenzake wa Simba, Mtawala ameula kwenye Mkurugenzi wa Sheria na Masuala ya Utawala ambayo ni nafasi mpya katika shirikisho hilo.
Kufuatia uteuzi huo ni wazi Mtawala atalazimika kuachia ngazi katika nafasi yake ya ukatibu kwenye klabu ya Simba, huku taarifa zilizoifikia Mwanaspoti usiku wa jana Jumatatu, Mtawala ameihakikishia TFF kwamba tayari ameshawasilisha barua yake ya kuacha kazi kwenye klabu ya Simba.
Mwesigwa na Mtawala watatangwa rasmi leo Jumanne na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.