Habari na Bin Zubeiry.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ amewashauri viongozi wa klabu yake ya zamani, Yanga SC kuwashirikisha wachezaji wake wa zamani katika uongozi ili kusaidia masuala ya kitaalamu.Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Makumbi aliyekuwa akifahamika pia kwa jina lingine la utani kama Bonga Bonga alisema kwamba watu wenye fedha ni muhimu katika klabu, lakini hata wataalamu ni muhimu pia.
Makumbi amesema Yanga SC hivi sasa ina hali nzuri kiuchumi kutokana na kuwa na viongozi wa wenye fedha kama Mwenyekiti wake Yussuf Manji na baadhi wa Wajumbe kama Abdallah Bin Kleb, Seif Ahmed ‘Magari’, Mussa Katabaro na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, lakini inakosa wataalamu wa masuala ya kiufundi.
Pesa si kila kitu; Makumbi Juma akizungumza na BIN ZUBEIRY jana |
Amesema Yanga ina utajiri mkubwa wa wataalamu, lakini viongozi wa klabu hiyo wameshindwa kuutumia na ndiyo maana pamoja na utajiri wao wanakwama kuwa na timu bora.
“Kuna wachezaji wengi wa zamani wenye mapenzi na Yanga na ambao pia ni wanachama, lakini hawashirikishwi na ndiyo maana timu inashindwa kufanya vizuri. Lazima tushirikishwe kwa sababu sisi tunaujua mpira na tumeucheza, wao wawezeshe mipango ya fedha, na sisi tutengeneze mambo ya kitaaamu, mambo yawe mambo,”alisema Bonga.
Wakali wa enzi hizo; Kutoka kulia Thomas Kipese, Paschal Kaliasa na Mohamed Hussein, wachezaji wa zamani wa Yanga SC |
Alisema; “Hawataki kabisa kusikia wachezaji wa zamani wa Yanga katika mfumo wa uongozi, hicho kitu siyo sawa, kuna mambo ambayo yanahitaji utaalamu, lakini pia hata nidhamu ya wachezaji imekuwa mbovu kwa sababu hawajui historia ya klabu wala magwiji wake,”.
“Leo hii mchezaji wa Yanga hamjui hata Sunday Manara ni nani wala Mohamed Huusein ni nani, kwa sababu viongozi hawathamini wachezaji wa zamani. Mimi wakati nasajiliwa Yanga (miaka ya 1980) nilipoingia pale klabuni nilikuta picha za wachezaji waliotutangulia akina Leonard Chitete, Maulid Dilunga na wengine na vikosi pia, lakini leo ukiingia Yanga hukuti hata picha ya kikosi cha msimu uliopita, haya ni makosa sana,”alisema Bonga.
Bonga amesema anawaheshimu viongozi wa Yanga, lakini lazima ufike wakati waienzi historia ya timu na magwiji wake ndiyo hata wachezaji watakuwa na nidhamu na kuithamini klabu.
“Leo pale Yanga kuna wachezaji wanajiona wanacheza mpira mkubwa sana, lakini ukweli ni kwamba hawajafikia uwezo wa wachezaji tuliowatangulia, ila kwa sababu klabu haina kumbukumbu za wachezaji wa zamani, basi Yanga inaonekana timu ya leo leo tu,”alisema. Hoja za Makumbi ziliungwa mkono na wachezaji wengine wa zamani wa Yanga, washambuliaji Thomas Kipese ‘’Ucle Thom na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ambao walimalizia soka yao kwa mahasimu, Simba SC aliokuwa wakati anazungumza.“Haya anayozungumza Bonga ni ukweli kabisa,”alisema Uncle Thom. “Lazima viongozi wa Yanga wawashirikishe wachezaji wa zamani, hata sisi tulipoingia pale Yanga tuliwakuta wachezaji wa zamani katika mfumo wa uongozi, kwa nini leo hawapo?”alihoji Mmachinga.