Dar es Salaam, Tanzania.Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rosweeter Kasikila (60) aliyeolewa na kinda wa miaka 26, Michael Christian, amegoma kutoa vyeti vya shule vya kijana huyo na kumtaka arejee nyumbani ili waendelee kuishi kama wanandoa.
Msimamo wa mbunge huyo umekuja baada ya kinda huyo kutumia kila mbinu akitaka arejeshewe vyeti vyake halisi vya shule ambavyo vimeshikiliwa na mbunge huyo kama njia ya kumshinikiza warudiane.
Habari zinasema kuwa taarifa ya ndoa hiyo iliyofungwa kwa siri na kuibua gumzo nchini, mara baada ya kuripotiwa na gazeti la Tanzania Daima, ndugu, marafiki na majirani wa mbunge huyo walimtaka aivunje na kurejesha kila kitu cha kinda huyo ili kuepukana na aibu Zaidi mbele ya jamii.
“Mbunge huyo ni mama yangu, tuliposikia habari za ndoa yake na huyo kijana, sisi kama familia tulishtushwa na kuhuzunika sana. Tulikubaliana naye kwenye vikao vya familia avunje ndoa hiyo na amrejeshee kijana huyo kila kitu, lakini hadi sasa amekaidi na ninasikia anafanya kila awezalo kutaka warudiane na kijana huyo,” amedokeza mmoja wa familia.
Michael amesema ametumia mbinu zote kutaka arejeshewe vyeti hivyo, lakini mbunge huyo amekataa kwa madai bado kinda huyo ni mume wake.
“Unajua kaka, kwa muda mrefu, ndoa yangu na mama imevunjika, hatuishi pamoja, na mimi nina mchumba mwingine ninaishi naye na mama anaendelea na maisha yake.
“Shida yangu kubwa kwake ni vyeti. Anaweza kubaki na nguo zangu na kitu kingine chochote, lakini vyeti vyangu ni muhimu kuliko maelezo. Kila ninapotafuta kazi au kutaka kujiendeleza kimasomo, sina vyeti, sipati nafasi ya masomo ya juu. Kupitia gazeti la lenu (Tanzania Daima) namuomba anirejeshee vyeti vyangu,” amesema Kinda huyo.
Michael ameweka wazi kwamba hayupo tayari kurejea kwa mbunge huyo na anaamini hana ndoa kwa kuwa ndoa aliyoifunga naye ni batili.
Kinda huyo amesema amewasiliana na vingozi mbalimbali wa dini na pia amemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani kutaka arejeshewe vyeti vyake bila mafanikio.
Naye Mbunge huyo amesema kwamba hayuko tayari kurejesha vyeti hivyo kwani bado anatambua Michael ni mumewe wa ndoa.
“Tangu lini umesikia ndoa ya Kikristo inavunjika? Lakini siko tayari kuzungumzia mambo haya kwenye magazeti,” amesema mbunge huyo kwa kifupi huku akikataa kuzungumzia ndoa yake na kinda huyo.
Mbunge huyo na Michael walifunga ndoa katika Kanisa la Mikocheni B, Mlima wa Moto, linaloongozwa na Mchungaji Getrude Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndoa hiyo ilifungwa Septemba Mosi mwaka 2011 na kubaki kuwa siri kabla ya wanandoa hao kukorofishana na kila kitu kikawa wazi. Source: Tanzania Daima.