JUMANNE, JANUARI 21, 2014 04:48 NA WAANDISHI WETU
*Ni kwa uamuzi wa kurudisha mawaziri mizigo
*Kikao kizito chafanyika Dar
UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kuwarudisha mawaziri watano wanaodaiwa kuwa mzigo ndani ya Baraza la Mawaziri, umeonekana wazi kuwasononesha vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Juzi Rais Kikwete alitangaza baraza jipya na kuwarudisha mawaziri hao, ambao wamekuwa wakipigiwa kelele na watu wengi, akiwamo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Mawaziri mizigo waliorudishwa na kuapishwa jana ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye ameapishwa kuwa Waziri wa Fedha.
Habari za kuaminika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana, zinasema kutwa nzima Kinana na wasaidizi wake wa karibu walikuwa na kikao kizito kujadili uamuzi wa Rais Kikwete wa kuwarudisha mawaziri hao.
“Ndugu yangu tumechanganyikiwa na uamuzi wa Rais wa kuwarudisha mawaziri hawa, tunaendelea na kikao chetu ambacho tunaamini kitatoa mwelekeo wa suala hili,
“Tumechanganyikiwa kwa sababu suala hili tulilichukulia uzito mkubwa kutokana na ziara ya Katibu Mkuu hivi karibuni… baada ya kubaini madudu yanayofanywa tuliamua kwa kauli moja kumpelekea mwenyekiti wetu majina ya mawaziri mizigo, sasa hakuna mabadiliko yoyote,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho, kilisema uamuzi wa Rais Kikwete kuwarudisha kwenye baraza hilo, unaweza kuzua mjadala mzito wa kitendaji kwa Kinana, ambaye alitoa msisitizo wa mawaziri hao kushughulikiwa.
“Hatujui nini ambacho tutakwenda kuwaeleza wananchi tena, tupo kwenye wakati mgumu, ngojeni tumalize kikao chetu tutawaambia tu tulichoafikiana,” kilisema chanzo chetu.
Mwaka jana, Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walifanya ziara ya siku 22 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe na kuwahakikishia wanachama wao kwamba mawaziri mizigo lazima washughulikiwe.
Baada ya ziara hiyo, mawaziri hao waliitwa mbele ya Kamati Kuu (CC) na kuhojiwa mbele ya Rais Kikwete mjini Dodoma.
WENGI WAKOSOA
Katika hatua nyingine, wasomi na watu wa kada mbalimbali wameendelea kukosoa Baraza la Mawaziri.
Ukosoaji huo, jana ulianza kutolewa na Tawi la Afrika Kusini, ambalo limeahidi kuwaundia tume kwa ajili ya kufuatilia utendaji wao.
Mwenyekiti wa tawi hilo, Kelvin Nyamori, alisema kikosi kazi hicho hakitahusiana na Serikali, bali kitajitegemea na kitatenda haki kwa kutoa taarifa za utendaji wa mawaziri na makatibu.
“Tutamfikishia Rais taarifa baada ya kufanya tafiti mbalimbali na hali hiyo itasaidia kuepusha suala la mawaziri kujiuzulu, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.
“Mfano katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo yupo Dk. Hussein Mwinyi, tayari alishawahi kuwapo pale na utendaji kazi wake haukuwa mzuri, je, tutegemee nini katika sekta hiyo?
Pia alihoji uteuzi wa Dk. Asha Rose Migiro, ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kwamba aliondolewa baada ya utendaji wake kutoridhisha, hivyo anaweza akashindwa kumudu kuiongoza Wizara ya Sheria na Katiba.
Wasomi
Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema kubadilishwa kwa mawaziri katika Wizara ya Katiba na Sheria, kunaweza kuufanya mchakato wa Katiba mpya kukosa mwelekeo.
Baregu alisema waziri aliyeteuliwa juzi ni wa tatu tangu kuanza kwa mchakato, jambo ambalo linaweza kuathiri mwelekeo.
“Dk. Migiro ana uwezo mkubwa, lakini anakuwa wa tatu kusimamia mchakato huo.
“Kutenguatengua mawaziri kunaweza kufanya mchakato usieleweke unakwenda wapi na unaweza kukosa mwelekeo endelevu,” alisema Profesa Baregu.
Pia alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipaswa kuwekwa kando kwanza, kwa sababu tuhuma zilizoainishwa kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili zilitokea wakati yeye akiwa kwenye wizara hiyo.
Baraza la Vyama
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray, alisema kutoondolewa kwa baadhi ya mawaziri walioonekana kuwa mizigo hakujawatendea haki wananchi waliokuwa wakiwalalamikia.
“Rais anatakiwa aendelee kuwasikiliza wananchi wanaozilalamikia hizo wizara na afanye utafiti wa kina.
”Na hata hao wapya wanatakiwa wapunguze ukada na siasa wachape kazi, kwa sababu utendaji unahitaji akili zaidi kuliko ukada,” alisema Mziray.
Chama cha Walimu
Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hakitegemei kama mabadiliko hayo yatakuwa na tija kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa sababu imekuwa ikitengewa fedha kidogo.
Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema hata kama Waziri Dk. Kawambwa angeondolewa, kusingeleta mabadiliko yoyote, kwa sababu bajeti bado ni ndogo.
“Kuchaguliwa kwa Jenista Mhagama kuwa naibu waziri, naona Rais Kikwete hakukosea, nategemea ataleta mabadiliko kama atawezeshwa,” alisema Oluoch.
Viongozi wa dini
Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya Pentekoste nchini, Askofu Dk. Philemon Tibanenason, alisema kinachotakiwa ni kuwapa ushirikiano mawaziri hao ili waweze kutimiza majukumu yao.
“Karibu wote waliochaguliwa mimi naona wanafaa, kilichopo ni wananchi kuwapa ushirikiano na viongozi wa dini tunatakiwa tuendelee kuwaombea kwa sababu uongozi siyo jambo dogo,” alisema Dk. Tibanenason.
↧
LIVE FROM GAZETI LA MTANZANIA SOMA WALICHOSEMA KUHUSU MAWAZIRI WAPYA LIVE!!
↧