Kila kukicha tumekuwa tukisikia taarifa mbalimbali za wasanii wa Bongo Fleva kusaini mikataba ya kwenda kufanya shoo katika nchi za Ulaya. Baadhi ya wasanii hao wa Bongo Fleva wamekuwa wakitangaza shoo hizo pasipo kueleza ukweli wa mikataba wanayoingia.
Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kuwa miongoni mwao wamekuwa wakienda kufanya shoo bure, huku wakiambulia kubadilisha mazingira ya hali ya hewa na kutakasa macho kwa kufika katika nchi hizo zilizoendelea.
Mmoja wa wasanii hao ni MB Dog ambaye sasa anakiri kutokunufaika na ziara hizo, baada ya kuzamia Ujerumani na baadaye Uingereza kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya kurejea nyumbani.
Vyanzo vyetu vya habari vinaonyesha kuwa, kumekuwepo na mawakala nje ya nchi, ambao wamekuwa wakiwaalika wasanii hao kwa makubaliano ya kuwalipia nauli tu ya kwenda na kurudi.
Starehe lilimtafuta mmoja wa mawakala kutoka nchini Uingereza maarufu kwa jina la Steve, ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana kwa simu, lakini likafanya mahojiano na baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kutaka kujua ukweli kuhusu ziara hizo za nje ya nchi.
Siku chache zilizopita msanii Chege Chigunda kutoka kundi la Wanaume Family, ambaye alisema kuwa kwake safari hizo amekuwa akizifanya kwa lengo la kutafuta fursa tu. Anasema kuwa katika shoo nyingi za nje, wengi wa wasanii wamekuwa wakizifanya bila masilahi yoyote.
“Unajua siyo kila safari lazima msanii utegemee masilahi ya kifedha tu, shoo zinatofautiana, zipo zenye masilahi ya fedha ila kwa hizi za Ulaya ni ‘exposure’ (Fursa) tu,” anasema Chege.
Hali halisi inavyokuwa
Kwa upande wake, Jhikolabwino Manyika maarufu kama Jhikoman naye ni mmoja kati ya wasanii wachache wanaopata mialiko ya nje ya nchi na kufanya matamasha nchi mbalimbali duniani kupitia muziki wa asili na reggae anaoufanya kwa muda wa miaka 12 sasa, anasema kuwa wasanii hao wamekuwa wakienda Ulaya kufanya shoo, nyingi zikitumia sebule kuwa ukumbi husika, iwe kwa malipo au bila malipo.
“Wasanii hawa hufanyiwa mipango na mawakala ambao ni kama madalali wa Ulaya. Msanii mwenye nyimbo yake iliyofanya vizuri Bongo, basi anaingia mkataba, inaweza kuwa bure bila hata malipo. Kinachofanyika ni kwamba, atalipiwa nauli ya kwenda na kurudi tu,” anasema Jhikoman na kuongeza: “Akifika huko, ukumbi atakaofanyia shoo ni chumba kidogo kitachokuwa kimekusanya Watanzania wachache wanaoishi huko, akirudi hapa nyumbani tunaambiwa alikwenda Ulaya kufanya shoo.”
Jhikoman anasema kuwa jambo hilo ni fedheha na aibu kwa wasanii wa Tanzania, akiongeza kwamba tatizo la Bongo Fleva kukosa mashabiki nchi za Ulaya linatokana na aina ya muziki wanaoufanya.
”Bongo Fleva ni kopi ya muziki wa Ulaya, hivyo wakifika huko wanaonekana hakuna kitu kipya kwa sababu wanachofanya ni sawa na wanachokifanya wasanii wao tena kwa ubora zaidi,” anasemaAnaongeza: “Mimi siwalaumu wasanii, ila chanzo ni wadau na vyombo vya habari ambao wamekuwa wakiwapumbaza na kwafanya waamini kwamba muziki wao unakua. Ni wachache sana ambao wanajitahidi kwa mbinu zao kuendelea.”
Kwa upande wake, Mrisho Mpoto anasema kuwa muziki wa Bongo Fleva, unawadanganya wasanii kutokana na presha za vyombo vya habari.
“Mimi naweza kusema kuwa hapa nchini sikubaliki kama ilivyo kwa nchi za Ulaya, hali hiyo inatokana na kukubalika kwa kazi zangu. Ni kwa sababu ya tofauti iliyopo kati ya muziki wangu wa asili na Bongo Fleva,” anasema Mpoto.
Mpoto ambaye ameteka soko na mialiko mbalimbali kutoka taasisi, wizara, asasi na mashirika anasema kuwa mbaya zaidi ni kwamba wengi wa wasanii hao hawajajitambua kwa muziki wanaoufanya.
“Wasanii wetu hawa mimi nadhani wamezaliwa kwa ajili ya kufanya muziki wa aina hiyo, bado hawajatambua wanapaswa kufanya nini ili kukuza muziki wao,” anasema.
Profesa Jay afafanua
Naye Profesa Jay anaizungumzia hoja hiyo katika mitazamo miwili tofauti akisema kuwa; kwanza muziki wa nyumbani (Bongo), bado haujafikia kiwango cha kuwa na shoo kubwa tofauti na zinazofanyika sasa nje ya nchi. “Bado muziki wetu hatujafikia ‘level’ (kiwango), kama za P Square, ambao wanaweza kufanya shoo kubwa Ulaya,” anasema Jay na kuongeza:
“Sababu kubwa inayokwamisha ni pamoja na wasanii wengi kukosa ubunifu. Unaweza kuwachukua wasanii 10 kwa sasa, wakafanana kila kitu wanachoimba, yaani wanafanya ‘kucopy’ (kuiga), tu. Kwa jinsi hiyo, muziki hauwezi kufika mbali.”
Jay anasema kuwa pamoja na udhaifu huo jambo la pili ni vyombo vya habari kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuutangaza muziki wa Bongo Fleva kama inavyofanyika kwa wasanii wengine wa Nigeria
“Nigeria wanafanyiwa ‘promo’ kubwa na hawana muziki wa kushangaza lakini; ‘media’ zetu zinapromoti mambo ya ajabu kabisa, uchafu tu,kwa hivyo hakuna nafasi muhimu kama mchango wa media kwenye kukuza muziki wetu,” anasema Jay.
Mbali na mazingira hayo Jay anapingana na kauli ya Chege akisema wasanii wanatofautiana thamani zao.
“ Pamoja na kufanya shoo hizo huwezi ukasema wote tunafanya ili kutafuta ‘exposer’, kwa mfano mimi na Chamilione ni kitu ambacho hakiwezekani kufanya shoo za bure,” anasema Jay.
Waliogoma kwenda Ulaya
Starehe imezungumza na baadhi ya wasanii ambao baada ya kubaini shoo za aina hiyo waliamua kutokwenda kabisa hadi pale masilahi na faida zitakapoanza kuonekana.
Mmoja kati ya wasanii hao ni pamoja na Izzo B ambaye anasema kuwa kwa upande wake ametambua kuwa shoo za hapa nyumbani zinamlipa vizuri kuliko malipo na mikataba ya kwenda Ulaya.
“Mapromota wengi wananifuata, lakini siko tayari kwa sababu sioni tofauti na shoo za hapa nyumbani, nitakuwa tayari kwenda nje endapo nitapata mikataba mizuri tofauti na hivyo sitakwenda kamwe,” anasema. Roma Mkatoliki naye anaeleza kuwa wasanii wengi huchukuliwa na kufanya shoo za bure kwa sababu ya ushamba wa kutembelea Ulaya.
“ Wengi wanakwenda kucheza shoo bure, wanalipiwa tiketi ya kwenda na kurudi tu, faida yake ni kutembea na kupata fursa ya kuona mazingira tofauti,” anasema na kuongeza;
“Siwezi kufanya shoo kama hizo kwa sasa mpaka nitakapoona kuna faida, yaani ni bora niende Mafinga kwa shoo yangu itakayonilipa 7 milioni saba kwa mara moja kuliko kwenda kuimbia watu bila malipo.”
SOURCE: MWANACHI
SOURCE: MWANACHI