- SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI
Dk Wayne Dyer, mtaalamu wa masuala ya uchumi na mwandishi wa vitabu katika kitabu chake cha Ufanye nini ili kupata unachokiazimia anasisitiza kuwa Mtafutaji makini huwa hachoki.
Hata hivyo, kuna vijana wengi nchini wanaonekana wamekata tamaa; Wengine hufikiri kwamba kama umezaliwa katika familia duni, maana yake utakuwa na maisha duni milele, huku wale ambao wamezaliwa katika familia tajiri, wanafikiri wataendelea kuwa tajiri.
Ukweli ni kwamba mtu yeyote anaweza kuwa na maisha bora, kama anavyosema msomi Hope Clark katika kitabu chake cha masuala ya Fedha kuwa siri ya kufanikiwa katika maisha ni kuishi kwa malengo, kuishi vizuri na watu na kupenda kuwa karibu na wasiokata tamaa.
NENO LA LEO
Tumekuwa tunaandika mara kadha kwenye NENO LA LEO kuhusu umuhimu wakujituma na kutokukata tamaa katika maisha. Ni ukweli ambao umethibitisha na watu wengi kwamba PENYE NIA PANA NJIA ili mradi uwe na MALENDO, UTHUBUTU WA KUTENDA, BIDII NA MAARIFA YA KAZI na KUMTEGEMEA MUNGU.
Kati ya vijana ambao wanaonekana kupambana hadi kuweza kujenga majina na heshima zao Duniani ni SALIM KIKEKE; ni mtu ambaye kama angekata tamaa hakika asingefika aliko sasa.
Sasa amekuwa ni mtu wa kujadiliwa na umaarufu wake hauko tu Tanzania, bali maeneo mengi ya Dunia hasa kunakozungumzwa Kiswahili. Huyu mtu ni kati ya watangazaji wakongwe na kivutio cha watu wengi kutoka barani Afrika na duniani kote, lakini katokea wapi?
SALIM KIKEKE NI NANI?
Salim ni Mtanzania anayetangaza vipindi mbalimbali katika Shirika la Habari la Uingereza (BBC). Safari ya kufikia mafanikio hayo ilikuwa na milima na mabonde, tabu na karaha.
Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke.
SALIM AAMUA KUWA MWANA-APOLO
Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.Kwa karibu mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi.
Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini. Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es Salaam.
Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake, Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Mboya ndiye mmoja kati ya rafiki zangu ambao tulibadilishana mawazo, tulifarijiana na kufikiria matarajio ya ndoto zetu, mambo yalikuwa magumu mpaka nikafikia hatua ya kusema basi imetosha,” anasema Kikeke.