Uongozi wa Klabu ya Simba umeweka wazi kuwa suala la kumuongezea mkataba kocha wake mkuu wa sasa, Zdravko Logarusic limewekwa pembeni kwa kuwa wanasubiri kuona mwelekeo wa timu yao ambayo imekuwa haina matokeo mazuri hivi karibuni.
Loga raia wa Croatia alisaini mkataba wa miezi sita wakati alipotua klabuni hapo mwishoni mwa mwaka jana, ambapo mkataba huo unatarajiwa kufikia tamati Juni mosi, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliweka wazi kuwa matokeo ya timu katika mechi zilizosalia ndiyo yatapa picha uongozi juu ya kuongeza au kutoongeza mkataba huo.
“Mkataba wake unatarajiwa kufikia tamati Juni mosi, mwaka huu tutaendelea naye mpaka mwisho wa ligi, makubaliano yetu ya awali yalikuwa ni kumpa mkataba wa muda mfupi ili kumuangalia na iwapo atafanya vizuri na kuridhisha basi tutamuongezea.
“Lakini suala hilo litaamuliwa mwisho wa ligi kwa wanachama na viongozi kutathmini kile alichokifanya na kama kubaki ama kutobaki ni maamuzi yatakayotolewa hapo baadaye,” alisema Kamwaga.
Simba inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo hivi karibuni iliambulia pointi mbili kati ya 12 ilizotakiwa kuzipata katika mechi nne za ligi hiyo