Kwa siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimetoa taarifa kuhusu kuvuliwa uongozi kwa Dkt. Kitila
Mkumbo ndani ya chama cha siasa kiitwacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Dkt. Mkumbo alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA. Taarifa hizo zimeushtua uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu zimekuwa tofauti na ilivyokuwa ikieleweka kuhusu uhusiano uliokuwepo baina ya Dkt. Mkumbo na CHADEMA.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa, kwa mujibu wa Waraka wa Mkuu wa
Utumishi wa Umma uliotolewa mwaka 2000 ni marufuku kwa mfanyakazi wa umma kuwa kiongozi, au kuwa na madaraka
yanayofanana na uongozi, katika chama chochote cha siasa. Kwa upande mmoja, Waraka huo uko wazi na wafanyakazi
husika wanaufahamu, na wale wanaoonyesha dalili za kutetereka hukumbushwa au kuonywa; wanaokaidi huchukuliwa hatua
kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Kwa msingi huo, na kwa kuzingatia kuwa Dkt. Mkumbo hajawahi kujibainisha rasmi kama
kiongozi ndani ya CHADEMA, Chuo hakikusita kumpitisha kuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha
Dar es Salaam kuanzia mwaka 2012. Kabla ya hapo, Dkt. Mkumbo alikuwa Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Taaluma
za Mitaala katika Shule Kuu ya Elimu, Kampasi ya Mwalimu Nyerere – Mlimani (2009-2012).
Kwa upande mwingine, pamoja na wingi wa taarifa hizo za vyombo vya habari, Dkt. Mkumbo amekanusha kimaandishi tuhuma hizo za kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, na kusisitiza kuwa yeye alijiuzulu nafasi hiyo ya ujumbe wa kamati kuu tangu Januari 2010, baada ya kutanabaishwa juu ya sheria husika, na kwamba hajawahi kuurejea wadhifa huo.
Baada ya kupata taarifa za vyombo vya habari zinazomhusisha Dkt. Mkumbo na nafasi ya uongozi katika CHADEMA,
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umelazimika kuchukua hatua ya dharura dhidi ya Dkt. Mkumbo, kwa
kumsimamisha kutoka kwenye nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo Chuoni. Lengo na manufaa ya hatua hii ni kama ifuatavyo.
Kwanza, kupitia kamati maalum iliyoundwa, Chuo kitapata fursa ya kufanya uchunguzi yakini utakaobainisha ukweli wa jambo
hilo. Pili, hatua hii itampa Dkt. Mkumbo fursa ya kujitetea katika ngazi zote zinazohusika, akiwa huru na bila kuathiri utendaji
kazi wa ofisi yake. Tatu, hatua hii itaiwezesha kamati husika, pamoja na Dkt. Mkumbo mwenyewe, kufanya kazi zao za
uchunguzi na utetezi bila kuingiliwa au kuathiriwa na cheo au madaraka aliyokuwa nayo Dkt. Mkumbo. Baada ya hatua hiyo,
Dkt. Mkumbo amemwomba Makamu Mkuu wa Chuo kwa maandishi amruhusu ajiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Kitivo na
ombi hilo limekubaliwa tarehe 3 Desemba 2013.
Pamoja na hayo, inabidi ieleweke kuwa Dkt. Mkumbo amejiuzulu uongozi, na siyo kazi; yeye bado ni mhadhiri mwandamizi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, izingatiwe kuwa suala la uchunguzi linaendelea, na kamati hiyo ya uchunguzi
imepewa jukumu la kuchunguza na kubaini ukweli, na kisha kutoa mapendekezo kwa uongozi wa Chuo. Mara baada ya
mapendekezo hayo, na baada ya Dkt. Mkumbo kupewa nafasi ya kujitetea na kusikilizwa, uongozi wa Chuo utatoa uamuzi
kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unauomba umma kuwa na subira katika jambo hili. Kadhalika, wale
watakaosailiwa na Kamati iliyoundwa tunawaomba watoe ushirikiano wa dhati ili kubainisha ukweli na kuharakisha mchakato
wa uchunguzi. Tunaamini kuwa penye ukweli, uwongo daima hujitenga, na hivyo katika hili, ukweli utadhihirika na hatimaye
haki itatendeka.
Imetolewa na
Prof. Yunus D. Mgaya
NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO - UTAWALA NA AFISA MNADHIMU WA CHUO KIKUU
3 Desemba 2013