Gari la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick likiwasili Dampo kuu la taka la Pugu Kinyamwezi, lililopo maeneo ya Gongo la Mboto jijini Dar alipofanya ziara ya ghafla kwenye dampo hilo.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na. Damas Makangale, MOblog
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick ametoa agizo mara moja kwa uongozi wa Dampo nje kidogo la jiji la Dar, Pugu Kinyamwezi, kurekebisha miundombinu ya barabara pamoja na taa ili kurahisisha umwagaji wa taka katika dampo hilo. MOblog inaripoti.
Akizungumza na baadhi ya viongozi wa wilaya na jiji hivi karibuni baada ya kufanya ziara ya ghafla katika maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa amesema tatizo la miundombinu ya barabara kuelekea katika Dampo la Pugu Kinyamwezi linasababisha foleni kwa malori ya kusomba taka katika jiji la Dar.
“mara ya mwisho wakati nakuja hapa kukagua hili dampo kulikuwa na taa na kazi ilikuwa inafanyika usiku na mchana sasa kumetokea nini,” alihoji Mkuu huyo wa Mkoa
Sadick aliagiza kwa viongozi wa jiji kushughulikia haraka tatizo la miundombinu ya barabara kuelekea Dampo ili kuongeza tija katika kazi ya kumwaga na kusomba taka katika jiji la Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Udhibiti taka kutoka halmashauri ya jiji, Bi. Enezael Ayo (kushoto) akifafanua jinsi magari ya taka yanavyomwaga taka katika dampo kuu taka la Pugu Kinyamwezi jijini Dar wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Dar.
Alisisitiza kwamba utaratibu mbovu wa umwagaji taka na miundombinu mibovu katika Dampo la Pugu Kinyamwezi vinasababisha mrundikano wa taka katika manispaa zote za Temeke, Ilala na Kinondoni.
Amesema kwamba ni muhimu kwa viongozi wa jiji kupata nguvu kazi ya kutosha ili kuwe na watu watakaosimamia umwagaji wa taka wakati wa usiku ili kudhibiti madereva wakorofi wanaomwaga taka ovyo bila kuzingatia taratibu.
Sadick aliongeza kuwa watendaji wa jiji ni lazima wawe na utaratibu wa kutoa mafuta kwa wakati kwenye magari ya kusomba (Bull Dozer) na vitendea kazi vingine.
Mkuu wa mkoa wa Dar, Said Meck Sadick akitoa agizo mara moja kwa uongozi wa Dampo nje kidogo la jiji la Dar, Pugu Kinyamwezi, kurekebisha miundombinu ya barabara pamoja na taa ili kurahisisha umwagaji wa taka katika dampo hilo. Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ndg. Raymond Mushi(mwenye suti nyeusi).
Wakati akitembelea maeneo kadhaa kati kati ya jiji kuanzia soko la Kisutu na mitaa ya Libya, Mkuu wa Mkoa aliagiza mamlaka zinazohusika kushughulikia haraka tatizo la maji machafu kupunguza harufu na kuzuia magonjwa ya mlipuko.
“nawaagiza mkae pamoja na mje na mpango mkakati utakaowezesha kumaliza tatizo la maji machafu yanayotoka katika mitaro na mifereji ya maji machafu katika ya jiji,” aliongeza
Wakati huo huo, wadau kadhaa wa usombaji taka katika jiji la Dar es Salaam wameomba serikali kutoa kipaumbele kwa Dampo la Pugu Kinyamwezi na kulitengea bajeti ya kutosha ili liweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tirima Enterprises, Bw. Robert Ngeleshi akizungumzia changamoto na matatizo ya mawakala wa kusomba taka katika jiji la Dar ambao waliongozana na Mkuu wa mkoa kwenye ziara hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Dar, Said Meck Sadick aliyeambata na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndg, Raymond Mushi wakiondoka eneo la tukio mara baada ya kuhitimisha zoezi la kukagua miundo mbinu ya Dampo la taka la Pugu Kinyamwezi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Minael Mshanga.