Dar es Salaam. Michuano ya Kombe la Kagame imepangwa kufanyika nchini Tanzania mwanzoni mwa mwezi Juni huku Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) likiwa kwenye mazungumzo ya mwisho na wadhamini wa michuano hiyo.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye
alisema jana kuwa kesho Jumatatu wanatarajia kumtangaza mdhamini wa michuano hiyo kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kumalizana naye.
alisema jana kuwa kesho Jumatatu wanatarajia kumtangaza mdhamini wa michuano hiyo kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kumalizana naye.
“Tupo kwenye mazungumzo ya mwisho na wadhamini wetu, nakuja huko Dar es Salaam kumalizana na wadhamini wetu, kila kitu tutaweka wazi Jumatatu, ngoja kwanza tumalizane nao,”alisema Musonye.
Cecafa imekuwa ikihaha kusaka wadhamini wa kuandaa michuano hiyo, ambapo awali walitangaza itafanyika Rwanda, lakini Rwanda ikawatolea nje kubeba gharama hizo, ambapo Cecafa wameamua sasa michuano ifanyike kwenye ardhi ya Tanzania.
Habari ambazo gazeti limezipata zinasema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo tayari kuisaidia Cecafa kubeba michuano hiyo kwa kuziingiza timu nne za Tanzania bara ambazo ni Simba, Yanga, Azam, na Mbeya City.
“Michuano hiyo inagharimu dola za Marekani 600,000 (Dola 1= Sh 1,594.90) na Cecafa haina kitu, TFF imezishauri iingize timu nne za Tanzania bara kwa vile zina mashabiki kwani Mbeya City ikicheza na Yanga au Simba zote zina mashabiki hivyo zitaingiza fedha za kutosha kuendesha mashindano hayo,”alisema kiongozi mmoja ndani ya TFF.
Katika michuano ya mwaka jana ambayo ilifanyika Darfur, Sudan, timu ya Vital ‘O’ ya Burundi ilinyakua ubingwa huku timu za Tanzania zikiwa zimejitoa.
Hata hivyo, kutokana na ukata unaoikabili Cecafa imebidi ikubali timu za Tanzania, Simba na Yanga kushiriki kwani zilijitoa kwenye michuano hiyo mwaka jana kutokana na kuzuiwa na Serikali kwa kile kilichoelezwa kuwa hali ya usalama katika miji ya El- Fasher na Kadugli huko Darfur siyo nzuri na kuzikataza timu za Simba na Yanga kwenda kushiriki michuano hiyo inayodhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kwa jumla ya dola za Marekani 60,000.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI