Jana (April 30), Kampuni ya Weusi ilizindua rasmi video ya wimbo wao ‘Gere’ pale Mediteraneo Hotel, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu wengi maarufu na mashabiki.
Uzinduzi huo ulifunguliwa kwa Live Show toka kwa wasanii waliowahi kushiriki Tusker Project Fame, Hisia na Damian Soul.
Hisia ndiye aliyeanza kufanya Live Show kwa gitaa na kuwapa zawadi watu waliohudhuria uzinduzi huo kwa kuimba wimbo ambao bado hajaurekodi unaioitwa ‘Give Me a Call’ na kuwataka watu wampe maoni kama aende akaurekodi au aachane nao.
“Kaurekodi…ingia studio.” Walisikika watu wakisema kwa sauti ya juu baada ya kuguswa na uimbaji mzuri wenye mguso wa wimbo huo wenye ujumbe wa mapenzi aka wimbo wa kitandani.
Ingawa wimbo huo uliimbwa kwa mara ya kwanza, watu waliweza kushika baadhi ya maneno ya kuitikia kuimba nae wakati anaurudia mara ya pili.
Hisia alifuatiwa na muimbaji wa muziki wa Soul Tanzania, Damian Soul ambaye aliwafanya watu waliohudhuria kuendelea kushangilia kama walivyofanya kwa Hisia. Damian aliimba nyimbo tatu, moja alirudia wimbo wa RnB wa Marekani na kufanya nyimbo zake mbili yaani ‘Ni Penzi’ na ‘Hakuna Matata’.
Baada ya show hizo, watu waliiangalia kwa mara ya kwanza video ya wimbo wa ‘Gere’ iliyoongozwa na Enos Olik nchini Kenya.
Video hiyo iliyotengenezwa kwa ubunifu wa kiafrika, inawaonesha rappers hao wakiwa katika muonekano wa mavazi ya kiafrika na wamejipaka rangi kama wanaoenda jando, huku warembo wakionekana pia katika muonekano huo. Lakini pia video hiyo imechanganywa na muonekano wa wahusika wakiwa ndani ya mavazi ya vijana wa kisasa.
Mchanganyiko huo na ubora wa hali ya juu wa uchanganyaji picha zenye muonekano mzuri, unatoa picha kuwa video hiyo inaweza kuonekana kwenye vituo vikubwa vya TV duniani muda si mrefu.
Ubora na ubunifu uliotumika kwenye video hiyo uliwafanya watu waombe irudiwe tena na tena…na kuoneshwa mara mbili.
Ilikuwa kama siku inaanza upya baada ya Weusi kupanda jukwaani kufanya ‘ukamilifu’ wa uzinduzi huo ambapo walifanya show nzuri iliyowafanya watu waliohudhuria kupiga kelele za shangwe mara kwa mara huku wakiimba kwa sauti pamoja na kundi hilo na kucheza hits kadhaa za Weusi.
Upendo uliooneshwa na watu waliohudhuria ulikuwa sehemu kubwa ya furaha ya Weusi ambao mara kwa mara walikuwa wakiwashukuru watu waliohudhuria na kuwaonesha upendo pia... “We love you guys... It’s too much. Tunawapenda sana yaani.” Joh Makini.
Baadhi ya watu maarufu waliohudhuria ni pamoja na Profesa Jay, Mwana Fa, AY, Ommy Dimpoz, Vanessa Mdee, Producer wa ‘Gere’ Nahreel na kundi lake ‘NavyKenzo’, Watangazaji wa Radio na Television Tanzania.