KATIKA kujitanua na kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, vyama mbalimbali vya siasa nchini, vimekuwa na mgawanyo wa jumuiya zenye lengo la kugawa makundi mbalimbali kwenye jamii.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM – Taifa, Mboni Mhita akijiandaaa kujibu hoja za waandishi wa habari katika ofisi za Global Publishers, sinza Bamaga.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina jumuiya tatu ambazo ni; Jumuiya ya Wazazi, Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Vijana (UVCCM). Kutoka Live Chumba cha Habari wiki hii, tunaye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM – Taifa, Mboni Mhita ambaye alizungumza mengi kuhusiana na jumuiya hiyo, hali ya kisiasa nchini na maisha binafsi kwa uchache. Mboni ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), aliye chini ya mwenyekiti wake Sadifa Juma, amejibu maswali ya wanahabari kama ifuatavyo;
LIVE: Siku za hivi karibuni, vijana wengi wamekuwa wakijiunga na vyama mbalimbali vya siasa hasa Chadema. Ninyi kama viongozi, hasa wewe mwenye nafasi ya juu kabisa katika jumuiya yenu, mmechukua hatua gani?
MBONI: Tumepokea vijana wengi sana kutoka upinzani. Lakini tumegundua kuna vijana wengi wanakuja kuchukua kadi wakitaka kujiunga nasi, lakini baadaye kadi hizohizo zinakwenda kutumika kwenye mikutano ya vyama vingine wakisema wanarudisha kadi za CCM na kujiunga nao.
Kitu ambacho hawajakijua, zile kadi zina namba za siri, tumeshagundua hilo. Ni propaganda za wapinzani. Hivyo siyo kweli sana kuwa vijana wengi wamekimbilia upinzani.
Lakini wanachama wanaojiunga nasi ni wengi zaidi ya wanaotoka. Ziara ya Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) ya nchi nzima imetuongezea wanachama wengi sana.
LIVE: Lakini pia, wasanii wengi hasa wa kizazi kipya wamekimbilia Chadema na wamegombea nafasi mbalimbali na kufanikiwa. Vipi kwa upande wenu CCM mmejipangaje? Angalia mfano mzuri, Sugu ‘Joseph Mbilinyi’, yeye aliingia Chadema na kutwaa Ubunge wa Mbeya Mjini.
Rudi kwa Renatus Pamba, alijiunga Chadema na akafanikiwa kuchukua Kata ya Sinza. Hivi karibuni, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’ amejiunga na Chadema.
Ninyi viongozi wa UVCCM mnalionaje?
MBONI: Tuna wasanii wengi mno walio UVCCM, isipokuwa chama chetu kina mfumo, huwezi kugombea nafasi yoyote mpaka uwe mwanachama ndani ya miaka mitano. Tumefanya hivyo kwa lengo la kuwaondoa watu wenye uchu wa madaraka.
Lakini huwezi kuwalinganisha vijana waliopo Chadema na kwetu. Sisi tuna vijana wengi wazuri tu bungeni; mfano tulikuwa na marehemu Amina Chifupa, sasa tuna January Makamba (Bumbuli - Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), Catherine Magige (Viti Maalum – Arusha), Deo Filikunjombe (Ludewa), Emmanuel Nchimbi (Songea Mjini), Sarah Msafiri (Viti Maalum – Morogoro)....
Huwezi kumfananisha Deo (Filikunjombe) na Afande Sele au ukamchukua Nchimbi ukamfananisha na Sugu, hivyo ni vitu ambavyo haviendani kabisa. Hata hivyo ukiangalia ni wazi kuwa wabunge wengi wa Chadema ni vijana waliokuja CCM wakaomba kadi, wakawa wanachama, wakaomba kugombea ubunge, taratibu zetu zikawabana, wakaondoka kwenda upinzani, wakachukua kadi wakagombea. Kwa hiyo kama tungekuwa tunataka hazina ya wabunge, Sugu alipoomba kugombea ubunge, tungekubali leo angekuwa mbunge kupitia CCM, lakini sisi hatuangalii hilo. Tuna misingi yetu ambayo ni kumfundisha na kumkuza kijana kwanza kabla hajagombea.
Miaka mitano utapikwa, utaandaaliwa kuwa kiongozi...huwezi kwenda kupigana ndani ya bunge ukiwa umeandaliwa kwa muda huo... nasikia Afande Sele atagombea mwaka 2015... namtakia kila la kheri.LIVE: Kwa nini UVCCM mpo kama vinyonga.
Unaweza kusikia mwenyekiti amesema kitu fulani, baadaye Makonda (Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi ) akazungumza kingine au kiongozi mwingine yeyote. Kwa nini hamna msimamo katika mazungumzo mbele ya vyombo vya habari?
MBONI: Wasemaji wakuu wa UVCCM ni mwenyekiti (Sadifa), makamu (yeye) na katibu mkuu (Sixtus Mapunda). Haijawahi kutokea tukapishana katika ya kwetu. Lugha inaweza kupishana lakini maudhui yatabaki yaleyale.
Wengine ni maoni yao tu, maana kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake binafsi, hivyo wakiongea siyo msimamo wa jumuiya yetu.
LIVE: Inasemekana kuna vijana walio UVCCM wamejiunga na kambi mbalimbali ndani ya chama. Unazungumziaje hilo?
MBONI: UVCCM hatuna kambi, binafsi sina kambi. Mimi ni mjumbe wa NEC na nadhani sisi ndiyo tutakuja na jina la atakayegombea urais. Mimi kama Mboni, sina kundi na jumuiya yetu kama taasisi ninayoiongoza haipo kwenye kambi yoyote.
LIVE: Nini faida na hasara za serikali mbili au tatu?
MBONI: Faida za serikali mbili ni nyingi; hasara zake mpaka sasa sijaona. Faida ya serikali tatu ni kwamba, itaneemesha baadhi ya watu wanaotaka nyadhifa.
Kutakuwa na marais watatu; Tanganyika, Zanzibar na Muungano, tutapata na ma - First Lady watatu, mabodigadi watatu, Ikulu nyingine ya tatu itaongezeka, kwa hiyo ajira zitaongezeka.
LIVE: Zamani kuwa mwanachama wa CCM kulikuwa na faida nyingi, mtu akitambulika aliheshimiwa na kupata huduma zote za kijamii kwa urahisi. Leo hayo hayapo.
Kuna faida gani ya kuwa mwanachama?
Mfano inawezekana vipi madereva bodaboda wanaandamana kwenda Ofisi za Chadema na siyo CCM? Kifanyeni chama kupitia UVCCM kiwe na nguvu kwa watu hasa vijana ambao ni wengi. MBONI: Naomba nipokee hili kama changamoto tuone namna ya kulishughulikia kama viongozi lakini bado naamini kuwa tuna ushawishi mkubwa kwa vijana wetu, tutajidhatiti zaidi.
-Global TV.