Ugonjwa wa homa ya dengue umezidi kusambaa mkoani Dar es Salaam na sasa umeathiri wilaya zake tatu na kuzua hofu kwa wananchi.Miongoni mwa walioathiriwa na homa hiyo ni mwanamuziki maarufu Rehema Chalamila (Ray C) ambaye amelazwa katika Wodi Namba Tano ya Hospitali ya Mwananyamala.Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, alithibitisha kulazwa kwa Ray C kutokana na ugonjwa huo jana.“Tumethibitisha kwamba Ray C ana dalili zote za dengue, lakini kimaadili siruhusiwi kutoa taarifa za mgonjwa,” alisema daktari huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Hata hivyo, waandishi wa gazeti hili walimwona mwanamuziki huyo hospitalini hapo akiwa katika usingizi mzito na madaktari walisema hakuwa katika hali mbaya bali alikuwa amelala kwa sababu ya uchovu wa dawa.
Mbali na Ray C, pia madaktari watatu na muuguzi mmoja wameripotiwa kuugua ugonjwa huo.
Tayari mamlaka zimetoa tahadhari kwa wananchi kuwataka wachukue hatua za haraka kuzuia maambukizi ya homa hiyo inayosababishwa na mbu anayejulikana kitaalamu kama aedes egyptiae.
Hadi sasa wagonjwa zaidi ya 100 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke na baadhi wakiripotiwa kupoteza maisha.
Takwimu kutoka Kitengo cha Utafiti wa Magonjwa cha Ifakara (IHI), kilichoweka kambi katika Hospitali ya Mwananyamala kutafiti aina za homa, zinaonyesha kuwa kwa miezi miwili ya Machi na Aprili pekee, wagonjwa 85 walibainika kuwa na homa hiyo.
Hata hivyo, idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na kukosekana kwa takwimu, vipimo na watu kuufananisha ugonjwa huo na malaria.
Daktari kiongozi wa hospitali hiyo ambaye pia ni mtaalamu wa ugonjwa huo, Dk Mrisho Rupinda alisema kuwa kuna taarifa za wagonjwa wa dengue walioripotiwa katika maeneo yote ya Dar es Salaam.
“Katika kipindi cha wiki moja iliyopita tayari madaktari wawili kwenye hospitali hii wamebainika kuugua ugonjwa huo, tunahisi walipata maambukizi kwenye maeneo ya humuhumu ndani hospitali,” alisema Dk Rupinda.
Alisema hali ni mbaya kuliko inavyodhaniwa kwa kuwa asilimia zaidi ya 50 ya wanaopimwa na kubainika kuwa na ugonjwa huo ni watu wazima kuanzia miaka 18.
Hata hivyo, takwimu za walio chini ya umri huo ni vigumu kupatikana kutokana na sampuli zinazopimwa na watafiti IHI.
Dk Rupinda alisema kuna wataalamu wa kutosha kubaini ugonjwa huo lakini tatizo kubwa ni vifaa na vitendanishi... “Mgonjwa anapobainika kuambukizwa dengue hana tiba rasmi, tunakutibu dalili.”
Amana na Temeke
Katika Hospitali ya Temeke jana wagonjwa walikuwa wakihamishwa katika wodi kwa ajili ya kupuliza dawa kudhibiti mbu.
Chanzo kimoja cha habari katika hospitali hiyo kilieleza kuwa, muuguzi na daktari mmoja wa hospitali hiyo waligundulika kuwa na homa hiyo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi wa homa ya dengue ambao walitibiwa na kuruhusiwa kwa kuwa hawakuwa mahututi.
“Ni ugonjwa wa mlipuko ambao huwa mkali kwa mara ya kwanza lakini baada ya watu kujua jinsi ya kujikinga, hupungua, pia muda ukipita mwili hujenga kinga wenyewe,” alisema Dk Shimwela na kuongeza:
“Kwa mfano, Aprili kuna kesi zaidi ya nne ambazo ziliripotiwa hapa kwetu.”
Alisema dalili za ugonjwa huo mara nyingi hufanana na zile za malaria kama vile homa kali, maumivu ya kichwa na misuli.
Msimamizi wa takwimu, maafa na dharura katika Manispaa ya Temeke, Dk Laurent Chipata alisema hali si shwari: “Kimsingi ugonjwa huu umelipuka kwa kiwango kikubwa sana kwenye Manispaa ya Temeke na hali ilivyo sasa inahitaji hatua za haraka kuwanusuru wakazi wake.” Alisema wagonjwa wote wanaofika wakiwa na homa wanapimwa kikamilifu na wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo wamekuwa wakipewa tiba.
Pamoja na mlipuko huo, alisema hakuna karantini iliyowekwa kwenye maeneo yote, bali wagonjwa wanaobainika hupewa usimamizi kuwekewa vyandarua kuzuia maambukizi zaidi.
Muhimbili
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilielezwa kuwa kati ya wagonjwa 10 wanaofika wakiwa na homa, wawili hadi wanne wanakuwa wameambukizwa ugonjwa huo.
Daktari wa magonjwa ya dharura na ajali katika hospitali hiyo, Juma Mfinanga alisema ugonjwa huo ulianza kubainika tangu Machi mwaka huu, hatua iliyosababisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuongeza nguvu ya kupambana nao.
Wizara ya Afya
Taarifa ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaeleza kuwa kuanzia Ijumaa wiki iliyopita hadi jana, wagonjwa 23 waliripotiwa katika Wilaya ya Kinondoni na sita Ilala.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja aliwataka wananchi kujifunza jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo na kuangamiza mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia dawa.
Kinga nyingine alisema ni kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile vifuu vya nazi, makopo na magurudumu ya magari, kufyeka vichaka, kufukia mashimo ya majitaka na kusafisha mazingira kwa jumla.
“Virusi vya homa ya dengue havina tiba maalumu wala chanjo, bali mgonjwa hutibiwa dalili zinazoambatana na ugonjwa huo kama vile homa, kupungukiwa maji au damu,” alisema Mwamaja.
Imeandikwa na Florence Majani, Andrew Msechu na Kelvin Matandiko.
MWANANCHI