Jeneza lenye mwili wa marehemu Daniel Lema kabla ya kuagwa. Marehemu Daniel Lema akiwa hospitali baada ya kuchomwa moto na wananchi. Ndugu wa marehemu wakiandaa jeneza kwa ajili ya mwili wa marehemu Daniel kuagwa. Daniel Anael Lema, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya sheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mt. Augustino, Tawi la Iringa (Ruaha University College - RUCO), amefariki dunia baada ya kushambuliwa kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira akidhaniwa kuwa mwizi.
Tukio hilo lilitokea Juni 24, 2014, majira ya saa 5 usiku ambapo inadaiwa kuwa Daniel alikuwa ametoka kuangalia michuano ya Kombe la Dunia, akawa anatafuta chakula cha jioni ambapo alipofika kwenye mgahawa mmoja ambao ulikuwa umefungwa, aliingia ndani ambapo binti aliyekuwa amelala ndani ya mgahawa huo, alianza kupiga kelele za mwizi zilizowakusanya wananchi wenye hasira kali.
Wananchi hao walianza kumshambulia Daniel wakiongozwa na mlinzi mmoja wa jamii ya Kimasai, baada ya kuzidiwa na kichapo wananchi hao walimmwagia mafuta ya taa na kumchoma moto kisha wote wakatoweka.
Mwanafunzi huyo aliokolewa na madereva bodaboda ambao walizima moto na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa lakini siku kadhaa baadaye alifariki dunia.
Mwili wa marehemu umeagwa mapema leo katika hospitali hiyo tayari kwa safari ya kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Jumatano.
Mungu na ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. AMINA!