Haruni Sanchawa, Dar
Zoezi la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mashine za Biometric Voters Registration (BVR) lililoanza juzi jijini Dar es Salam, limekuwa ni balaa kwa wakazi wake kutokana na matatizo mengi yaliyojitokeza hivyo kusababisha adha kwa wananchi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu juzi na jana katika vituo mbalimbali vya uandikishaji jijini Dar, umebaini kasoro nyingi ambazo zimefanya wananchi wanaokwenda kujiandikisha kutoa lawama kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayoongozwa na Jaji Damian Lubuva.
Katika Kata ya Chanika, wilayani Ilala, gazeti hili lilishuhudia jana maofisa wakifika kituoni wakiwa wamechelewa kwani saa mbili zoezi la uandikishaji lilikuwa bado kuanza huku wananchi wakiwa wamewahi kufika saa 11 alfajiri, hivyo kuzusha manung’uniko.
“Tumefika tangu saa kumi na moja alfajiri, lakini watendaji wamechelewa hii inaonesha ni jinsi gani Tume ya Uchaguzi ya Taifa haiku makini kusimamia watu wake,” alisema Rehema Abdallah.
Kero nyingine iliyolalamikiwa na wananchi ni ucheleweshwaji wanapoingia kwenye mashine hizo tatizo ambalo lilielezwa na mtaalamu mmoja wa mtandao (IT) aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji kwamba linachangiwa na vumbi.
“Tatizo linguine linasababishwa na wananchi wanaofika kujiandikisha, hujipaka mafuta katika viganja vyao, hivyo kusababisha mashine kutotambua alama zao,” alisema mtaalamu huyo.
Aliongeza kusema kuwa mashine hizo ni za kielektroniki, hivyo zinatakiwa kuwa safi hazipaswi kukutana na vumbi.
Katika Kituo cha Mwenge Mlalakua, wananchi wengi walilalamikia foleni kuwa ndefu na zoezi kwenda taratibu sana huku wakidai kuwa kuna makundi ya wazee wanaingizwa ndani na huchukua muda mrefu kutoka.
“Tulikuwa watu wengi sana hapa, zaidi ya mia tatu, lakini tukaambiwa wataandikishwa watu mia mbili tu kutokana na uwezo wa mashine. Hii ni mbaya na inakatisha tamaa,” alisema John Kijo mkazi wa Mwenge.
Gazeti hili lilifika Mitaa ya Kawe, Bunju, Sinza, Msasani, Kijitonyama na Kinondoni na kukuta matatizo ni hayohayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana alisema ana imani zoezi hilo litakwenda kama lilivyopangwa kwani uandikishaji huanza saa mbili hadi saa 12 jioni.
“Tangu juzi hadi jana hakuna taarifa yoyote iliyonifikia kuhusu uvunjifu wa amani au mtu kuharibu utaratibu uliokuwa umeandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, changamoto nyingine zitatatuliwa haraka,”alisema.
Jiji la Dar es Salaam lina jumla ya watu 4,713,217 kati yake wenye sifa ya kupiga kura ni 2,932,930 na lina Wilaya za Temeke, Kigamboni, Ubungo, Kinondoni na Ilala, huku majimbo yakiwa ni kumi baada ya Nec kuongeza majimbo mawili ya Mbagala na Kibamba.